Jiwe la maajabu la Mbuji lililopo katika Wilaya ya MbingaJIWE la Mbuji lililopo wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, ni miongoni mwa vivutio adimu na vya kipekee vilivyopo katika Bonde la Ziwa Nyasa ambalo linajumuisha mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Njombe.Tayari Wizara ya Maliasili na Utalii imeliingiza Jiwe la Mbuji kwenye orodha ya vivutio vya utalii vilivyoko mkoani Ruvuma ili hatimaye kazi ya kutangaza eneo hilo na vivutio vingine, iweze kufanyika kwa tija.Neno Mbuji lina maana ya Kitu Kikubwa. Hivyo pengine, jiwe hilo kuitwa Mbuji, ilitokana na ukubwa wake usiokuwa wa kawaida. Jiwe hili lipo katika Kijiji cha Mbuji, Kata ya Mbuji.
Kwa sasa limekuwa kivutio kwa wageni wa ndani na nje wanafika kutembelea wilaya ya Mbiga kwa shughuli zao mbalimbali, zikiwemo za kitalii.Moja ya maajabu ya jiwe hili, ni ukubwa wake likilinganishwana mawe yote yanayopatikana katika mkoa wa Ruvuma. Chini ya jiwe hili kuna vyanzo vingi vya maji. Ni vigumu kwa mtu yeyote kulipanda bila kwanza kuwaona wazee wa kimila wa eneo hili. Yeyote anayethubutu kulipanda bila kuwaona wazee hao, yanayomkuta anajua mwenyewe, lakini ukweli ni kwamba ni tayari juu yake. Ni vigumu kulizunguka jiwe hilo bila kufuata mila na desturi za Kabila la Wamatengo wanaoishi eneo hilo.Kwa jamii ya Wamatengo, jiwe hili linaheshimika sana.
Sehemu kubwa ya wananchi wanaoishi kuzunguka eneo lilipojiwe hili hawajawahi kulipanda wala kulisogelea katika maisha yao yote kwa hofu ya kupoteza maisha.Sixmund Ndunguru (90), ni mmoja wa wazee wa kimila wa Kabila la Wamatengo. Katika mazungumzo yake na FikraPevu anasema pamoja na mambo mengine kwamba ili kuweza kupanda jiwe hili, ni lazima mtu awe na mzee wa kimila wa kumwongoza, anayezifahamu vizuri mila na tamaduni za kabila hilo.“Ninayafahamu maajabu ya jiwe la Mbuji tangu nikiwa na umri mdogo. Mandhari ya jiwe hili hayajabadilika wala kuharibiwa tangu nilipoanza kulifahamu,” Mzee Ndunguru anaanza masimulizi yake juu ya jiwe hili.Anaendelea: “Mimea hii aina ya matete inayozunguka jiwe hiliimekuwepo miaka mingi sana. Kwa mara ya kwanza, mimi mwenyewe nilipanda juu ya jiwe hili miaka ya 1940 nikiwa na baba yangu mzazi…
kwa hiyo, mtu yeyote anaruhusiwa kupanda jiwe hili ilimradi azingatie maelekezo ya wazee wa kimila.”Kwa kawaida, Wamatengo wanaamini kwamba katika jiwe hili lina viumbe vinavyoitwa Ibuuta ambavyo ni mfano wa binadamu. Viumbe hivyo vinaelezwa kuwa vifupi mno na vya ajabu. Inadaiwa kwamba wakati mwingine inapofika usiku viumbe hivyo huweza kuonekana. Hata hivyo, inaelezwa kwamba viumbe hivyo vifupi vinapatikana pia katika mataifa kadhaa duniani, lakini vikifahamika kwa majina tofauti.Historia inaonyesha kuwa Jiwe ka Mbuji tangu zamani lilikuwa linatumiwa na wazee wa kimila kwa ajili ya kutambika.
Taratibu hizo za kutambika huambatana na watu kujipaka usoni unga wa mhogo. Unga huo hutumika hadi sasa kwa kumpaka yeyote anayetaka kupanda jiwe hili, wakiwemo wageni wanaotaka kupanda jiwe hili, kinyume na hapo mtu anaweza kupata matatizo mengi, ikiwemo kupoteza maisha.“Iwapo mtalii ataamua kupanda jiwe hili bila kuwaona wazee wa kimila, moja kwa moja atakuwa amevunja mila na desturi za jamii ya hapa, hivyo anastahili kupata adhabu,” anasisitiza Mzee Ndunguru.Baadhi ya Wazee wa mila katika kijiji cha Mbuji chenye jiwe lenye maajabu Wilayani Mbinga Mkoani RuvumaBaadhi ya Wazee wa mila katika kijiji cha Mbuji chenye jiwe lenye maajabu Wilayani Mbinga Mkoani RuvumaKwa mujibu wa Mzee huyo, mtu huweza kumchukua kati ya saa 12 na 14 kulimaliza jiwe hili, ingawa kwa muonekana wake kwa macho, mtu anaweza akadhani kwamba anaweza kumaliza kulizunguka hata kwa nusu saa tu.“Hii ndiyo moja ya maajabu yake. Kwa kuliangalia, mtu anaweza akadhani anaweza kumaliza kulizunguka kwa nusu saa tu, lakini ukianza rasmi kazi ya kulizunguka, inaweza kukuchukua saa 12 hadi 14…wengine wanashindwa na kukata tamaa na kuishia njiani,” anasimlia Mzee Ndunguru.
Uchunguzi umebaini kuwa mtu anapoliangalia jiwe hili la mbuji kwa mbali, linaonekana ni fupi, lakini kadri anavyolikaribiandivyo jiwe hilo linavyozidi kuwa refu. Hali hiyo ndiyo inafanya ugumu huo wa kulizunguka lote kwa muda mfupi. Aidha, Jiwe la Mbuji hutumika kuwaombea watu wanaosumbuliwa na mapepo. Watu wenye tatizo hilo hupandishwa juu ya jiwe hili na kuombewa kimila kabla ya mapepo hayo kuondoka na mgonjwa kupona kabisa.Takwimu zinaonyesha kmbawa kila mwaka, idadi ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wanatembelea jiwe hili ambalo lipo umbali wa kilometa 150 kutoka Songea mjini,yaliko Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma. Leodgar Kumburu(97) ni mzee mwingine wa kimila mwenye makazi yake kijijinihapo Mbuji. Katika masimlizi yake juu ya jiwe hilo, anasema zamani wazazi wake kabla ya kusafiri, walikuwa wanakwenda kwanza kuhiji katika jiwe hili pamoja na kuomba mambo mbalimbali kabla ya kuanza safari yao.“Mmoja wa watu waliowahi kupoteza maisha katika jiwe hili, ni mama mmoja ambaye alikuwa na mapepo. Alipanda jiwe hili akiwa peke yake, lakini akiwa kileleni tayari alianguka na kupoteza maisha huko huko juu…
kuna mtalii mwingine mmoja raia wa Marekani ambaye aliamua kupanda jiwe hili bila mwongozo wa wazee wa kimila. Huyu baada ya kupandana kufika katikati ya jiwe hili, alianza kusinzia na kuamua kushuka, lakini alianguka kabla ya kufika chini na kupoteza maisha yake,” anasimlia Mzee Kumburu akielezea matukio ya vifo vilivyowahi kuwapata baadhi ya waliojaribu kupanda jiwe hilo bila kuwaona wazee wa mila.Kwa mujibu wa Mzee huyo, mtalii huyo raia wa Marekani aliyefariki dunia baada ya kupanda jiwe hilo bila mwongoza wa wazee wa kimila, alikuwa yuko na mke wake ambaye aligoma kupanda baada ya kuanza kujisikia vibaya akiwa bado yuko chini.“Mtalii yule, baada ya kugomewa na mke wake, alichukua rozali yake mkononi na kuanza kusali huku akipanda jiwe hilo. Hata hivyo, rozali ile haikumsaidia kwani alipoteza maisha,” anasema Mzee Kumburu huku akisisitiza umuhimu wa kila mtalii kuwaona wazee wa kimila kabla ya kuamua kupanda katika jiwe hilo lenye maajabu.
Mzee huyo anabainisha kwamba kifo cha mtalii huyo raia wa Marekani, kulichochea idadi kubwa ya watalii kutoka nje kumiminika kwenda katika jiwe hili, baadhi yao kwa ajili ya kufanya utafiti uliolenga kubaini maajabu na nguvu ya miujizaya jiwe hilo. Kutokana na kasi hiyo ya ongezeko la watalii katika jiwe hili, Serikali ya Kijiji cha Mbuji kwa kushirikina na wazee wa mila, wameamua kuboresha mazingira ya eneo hilo kwa kujenga nyumba za kimila za jamii ya Wamatengo, ikiwa ni pamoja na kupika vyakula vya asili, kuunda vikundi vya ngoma za jadi na kadhalika ili watalii wakishaona jiwe hilo wanapata vyakula na kuangalia ngoma za asili ya Wamatengo hivyo wananchi kujipatia kipato.“Kuna wageni wengi watalii wanatembelea Wilaya ya Mbingakutoka nchi za Marekani na Ujerumani wanaopenda kuja kutalii hapa katika jiwe hili, na moja ya sababu inayofanya watalii hao waje kwa idadi kubwa ni pamoja na vifo viwili vya watalii wa kigeni kutoka katika nchi hizo, anasema Ngwatula Ndunguru, ambaye amewahi kuwa mbunge wa Mbinga.Kwa mujibu wa Ngwatula, ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wazee wa kimila kijijini hapo, mababu wa jamii ya Kimatengo walikuwa wakipanda jiwe hilo hadi juu kwa ajli ya kucheza ngoma za asili, zikiwemo ngoma za Mganda, Muhambo, Chioda na Limbetembe.Sheria ya Mambo ya Kale ya Mwaka 1964, kifungu cha 16 (1-2), na marekebisho yake ya mwaka 1979, inazipa Mamlaka za Miji na Halmashauri za Wilaya uwezo wa kuweka sheria ndogo ndogo ambazo zitatumika kuhifadhi, kulinda na kuratibu uingiaji katika maeneo yenye historia kama ilivyo katika Jiwe la Mbuji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.