BAADHI ya viwanda vya kukoboa kahawa katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,viko hatarini kufungwa kutokana na kupungua kwa uzalishaji na bodi ya Kahawa Tanzania kuruhusu makampuni na wafanya biashara binafsi kusafirisha kahawa kavu kwenda nje ya wilaya hiyo.
Wamiliki wa viwanda hivyo, wameiomba bodi ya Kahawa Tanzania kutoruhusu makampuni na wafanyabiashara hao kusafirisha kahawa ghafi(za maganda) ili kulinda viwanda vilivyopo katika wilaya hiyo badala yake kahawa yote ikobolewe kwenye viwanda vya Mbinga.
Wamesema,kama Serikali kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania itaendelea kutoa vibali katika msimu huu basi kuna uwezekano mkubwa wa viwanda vya Mbinga kufungwa kwa kukosa malighafi na hata kusababisha watu wengi hususani vijana kukosa ajira.
Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha kukoboa kahawa cha MCCCO Rabiel Ulomi alisema,wilaya ya Mbinga kuna viwanda vitatu vyenye uwezo wa kukoboa tani tani elfu hamsini,lakini tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa uzalishaji wa zao hilo haujafikia kiwango hicho.
Alisema,kiwanda cha MCCCO kina uwezo wa kukoboa tani 30,000 kwa mwaka ambapo katika msimu wa 2022/2023 kimekoboa tani 8,846 na kilo 647 chini ya malengo ya kukoboa angalau tani 10,000.
Alisema,hali hiyo imetokana na kushuka kwa uzalishaji na Bodi ya kahawa kuruhusu makampuni yanayonunua kahawa kutoka kwa wakulima kupeleka nje, badala ya kutumia viwanda vya ndani ya wilaya hiyo.
Alisema,hatua hiyo imeathiri sana viwanda vya Mbinga,uchumi wa wananchi wa Mbinga na wilaya hiyo ambao kwa kiasi kikubwa inategemea mapato na uchumi wake kutoka kwenye viwanda hivyo.
Ulomi ameishauri serikali kuhakikisha kuwa,kahawa inayolimwa Mbinga inaborewe kwenye viwanda vilivyopo katika wilaya hiyo badala ya kupelekwa nje na mkulima akishaingiza kahawa kiwandani aendelee na mchakato hadi siku ya mnada.
Mmiliki wa kiwanda kingine ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema,kama bodi ya kahawa itaendelea kuruhusu kahawa ya Mbinga kusafirishwa na kwenda kukobolewa nje,kuna uwezekano mkubwa wa viwanda vya Mbinga kufungwa.
Aidha,ameiomba serikali kupitia upya uamuzi wake wa kuruhusu jambo hilo,kwani lina madhara makubwa kwa wananchi na wilaya ya Mbinga ambayo inategemea zao la kahawa kama nguzo kuu ya kiuchumi.
Mmoja wa vibarua katika kiwanda cha MCCCO Daud Challe alisema,kama Bodi ya kahawa itaruhusu kahawa ya Mbinga isafirishwe na kukobolewa nje ya viwanda vya Mbinga,basi Taifa litegemee kuongezeka kwa vijana wengi wa mitaani ambao hawana ajira.Alisema utaratibu huo ukisitishwa,uchumi wa Mbinga utaongezeka na wananchi watapata ajira kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye viwanda vya kukoboa kahawa.
Kwa upande wake meneja wa Bodi ya Kahawa kanda ya Songea Peter Bubelwa alisema,kampuni inayolalamikiwa kununua na kusafirisha kahawa nje ya Mbinga,imepata vibali kutoka Halmashauri zote zinazolima zao hilo ambazo zimeridhia utaratibu huo.
“ni kweli kuna viwanda vitatu katika wilaya ya Mbinga vyenye uwezo mkubwa wa kukoboa kahawa yote inayozalishwa,lakini sisi kama bodi ya kahawa tumeruhusu kampuni hiyo(Aviv Ltd) ambayo ni mdau na mkulima mkubwa kununua na kusafirisha kahawa nje ili kuleta ushindani katika sekta ya kahawa”alisema Bubelwa.
Naye mtaalam kutoka Bodi ya kahawa Tanzania kanda ya Songea Rashid Membe alisema,kilio cha wamiliki wa viwanda vya kukoboa kahawa ni kuendelea kuwahimiza wakulima kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.