Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea (HOMSO) Dr. Charles Hinju, amesema wameungana na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi kutoa matibabu ya macho kwa wakazi wa Ruvuma.
Amesema huduma hizo zinazotolewa kwa gharama nafuu kupitia shirika la EyeCorps, kwa kushirikiana na madaktari kutoka CCBRT, Hospitali ya Kanda ya Mbeya, na Muhimbili zimeanza Novemba 11 na zitamalizika Novemba 20 katika hospitali ya Mkoa.
"Tunatoa huduma kwa gharama nafuu zaidi, watu walikuwa wanakuja kwetu na wanakosa huduma kwa kukosa kuchangia gharama, lakini hawa ndugu zetu na kwa kushirikiana na Serikali imeweza kutumia hii nafasi kupunguza gharama ndio maana watu wengi wamejitokeza kupata huduma," alisema Dr. Hinju.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha wiki moja kabla ya kuanza rasmi matibabu hayo madaktari walitembelea Vijiji vya Wilaya ya Namtumbo, Songea Vijijini, na Manispaa ya Songea, kuwachunguza wagonjwa na kufanikiwa kuwapata wagonjwa zaidi ya 1,000.
Amebainisha kuwa wanatarajia kufanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu 250, na huduma zingine kama kutoa miwani kwa wenye shida ya kuona, kusoma maandishi, na mwanga zinatolewa, hivyo wananchi waendelee kujitokeza ili waweze kufaidika na huduma hiyo.
Mmoja kati ya wagonjwa waliopatiwa huduma ya macho Florencia John kutoka Wilaya ya Tunduru amesema amefurahishwa na huduma aliyopatiwa kwa sababu alikuwa na tatizo kwenye macho yote mawili na ameshahudumiwa jicho moja na ameanza kuona, amewaomba watoa huduma kuendelea kutoa huduma hizo kwa kuwa sio kila mtu anaweza kulipia.
Naye Selemani Sindo kutoka Wilaya ya Namtumbo ameeleza kuwa jicho lake moja lililkuwa halina uwezo wa kuona lakini baada ya upasuaji sasa anaona vizuri kwa kutumia macho yote.
Huduma hii inayotolewa na kambi ya madaktari wa uchunguzi wa magonjwa ya macho huwa inatolewa kila mwaka ambapo mwaka 2023 wagonjwa 185 mkoani Ruvuma walipatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho, na mwaka huu wanatarajia kufanya upasuaji huo kwa watu 250.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.