Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, serikali, na wadau mbalimbali katika kupinga ukatili wa kijinsia na kuhakikisha haki za watoto na wanawake zinalindwa.
Amesisitiza hayo wakati akizindua siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo uzinduzi huo kimkoa umefanyika katika wilaya ya Namtumbo.
"Kama mkoa kwa pamoja tunatakiwa kuhakikisha tunapinga ukatili kwa nguvu zote, kila mzazi kutimiza wajibu wake kwenye malezi na kuhakikisha watoto wanapata haki zao bila kujali jinsia zao, mgawanyo wa kazi, fursa za kupata Elimu, kutoa ushauri na kusikilizwa viwe sawa," alisema Bi. Mary.
Ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kushiriki katika maamuzi na shughuli za kiuchumi bila kuathiri majukumu yao kama walezi wa familia, kwani watoto wamekuwa wakijilea wenyewe kwenye maeneo mengi ya mkoa wa Ruvuma, hali inayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama wa kutosha.
Bi. Mary amesema Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri lakini inakosa ushirikiano katika kutoa Elimu inayohusu ukatili wa kijinsia kwa sababu changamoto ya ukatili imekuwa ikiendelea.
"Upande wa Serikali tunafanya kazi nzuri sana lakini tunakosa ushirikiano kwenye kutoa Elimu na kushughulikia masuala ya ukatili kwani Elimu imekuwa ikitolewa lakini bado changamoto ya ukatili imekuwa ikiendelea, ni vyema sekta zote kuhakikisha zinafanya kazi kwa pamoja na mifumo isomane katika kushughulikia masuala ya ukatili," alisema Bi. Mary.
Kuelekea maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Bi. Mary amewahimizwa wadau kushiriki kwenye makongamano, mikutano, na mijadala kuanzia ngazi ya familia ili kujua hatua zilizopigwa na wapi palipokosewa ili kurekebisha na kuendelea kulinda haki za kila mmoja kwenye jamii.
Kauli mbiu ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka huu inasema "Kuelekea Miaka 30 ya Beijing: Chagua Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia," ambapo mwaka 1995 wanawake wapatao 51,000 kutoka nchi mbalimbali duniani walikutana nchini China kujadili na kuweka mikakati ya kumaliza ukatili wa kijinsia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.