Utafiti umebaini karibu kila wilaya iliyopo katika Mkoa wa Ruvuma ina vivutio mbalimbali vya utalii vinavyoweza kufungua milango ya utalii katika wilaya husika na kutoa ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo adimu hapa nchini na duniani kote.
Hebu tuone baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo vipo kila wilaya mkoani Ruvuma, tukianza na wilaya ya Nyasa mjini Mbambabay kuna fukwe, visiwa, samaki wa mapambo, hifadhi ya Ndengere, utalii wa michezo ya majini na majengo ya malikale ya makanisa ya Lituhi na Lundu.
Eneo la Liuli wilayani Nyasa kuna vivutio vya Jiwe la kihistoria la Pomonda, fukwe, samaki wa mapambo, historia ya kanisa la Anglikana Tanzania, michezo ya majini, ngoma za asili za kioda na mganda.
Katika eneo la Lundu wilayani humo, kuna vivutio vya jiwe la Chingata, fukwe za samaki wa mapambo, hifadhi ya misitu ya asili ya Lilengalinga, majengo ya historia, michezo ya majini na ngoma za asili.
Wilaya ya Mbinga,nayo imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vikiwemo bustani ya wanyama ya Lugari, jiwe la maajabu la Mbuji,kilimo cha Ngoro na pori la Liparamba ambalo linafaa kwa utalii wa picha,utafiti wa mimea na utalii wa uwindaji.Maeneo mengine ya utalii katika wilaya ya Mbinga ni Hifadhi.
Tukiangalia katika wilaya ya Songea,kuna Hifadhi ya Gesimasowa ambayo inafaa kwa utafiti wa aina mbalimbali, kuwinda na utafiti wa malikale,Hifadhi ya asili ya Luhira, Hifadhi ya Misitu ya milima ya Matogoro,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Makumbusho ya Mzee Kawawa na Pango la Mlima Chandamali ambalo lilikuwa maficho ya Nduna Songea Mbano wakati wa Vita ya Majimaji.
Vivutio vingine vilivyopo katika wilaya ya Songea ni Bwawa la Tulila, maporomoko ya Mto Ruvuma, majengo na majumba ya kihistoria likiwemo kanisa kongwe la Peramiho.
Vivutio vya utalii vilivyopo katika wilaya ya Tunduru ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kanda ya Kalulu linalofaa kwa utalii wa uwindaji, Hifadhi ya asili ya Mwambesi inayofaa kwa utalii wa picha na utafiti, eneo la utalii wa mambokale la Masonya na njia ya kusafirishia watumwa ya Mbatamila hadi Masonya ambako ilikuwa kambi ya wakimbizi na ofisi za vyama vya FRELIMO toka Msumbiji.
Katika wilaya ya Tunduru pia kuna njia ya watumwa ya Kusini iliyokuwa inapitisha watumwa toka Msumbiji kupitia mkoa wa Ruvuma hadi Mikindani mkoani Mtwara ambako kulikuwa na soko la watumwa.
Katika wilaya ya Namtumbo kuna vivutio vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Kanda ya Likuyuseka ambayo inafaa kwa uwindaji wa utalii na utalii wa picha na Mji mdogo wa Lusewa katika maeneo ya Kimbanda na Kisungule ambako kunafaa kwa utalii wa kuwinda na picha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.