MOJA ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve(Luhira zoo) yenye ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1974,ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.
Afisa Utalii wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) katika hifadhi ya Luhira David Tesha amesema Bustani nyingi za wanyamapori zilizopo mjini zimetengenezwa na binadamu(Artificial Game Reserve),lakini bustani ya wanyamapori ya Luhira ni ya pekee ya asili nchini iliyopo mjini.
Tesha amesema Luhira zoo ilianza kuhifadhiwa ikiwa chini ya Mkoa wa Ruvuma,mwaka 1990 baada ya kuanzisha Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU),eneo likachukuliwa kwenda katika Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Idara ya Wanyamapori na mwaka 2015 eneo hili likachukuliwa na TAWA chini ya usimamizi wa KDU.
Kulingana na Afisa huyo wa TAWA bustani ya Luhira yote imewekewa uzio na kwamba ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.
Amesema Luhira zoo ni eneo la asili lenye utajiri wa miti ya miyombo,misuku,mitumbitumbi,miwanga,minyonyo,mizambarau,mininga, na mikuyu,na kwamba ni miongoni mwa bustani chache zenye uoto wa asili kabisa zilizopo mjini.
“Ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum’’,alisema Tesha.
Amesema ndani Luhira zoo kuna mto Luhira ambao unatitirisha maji mwaka mzima na kuna maporomoko ya kuvutia hali ambayo inavutia watalii wengi ambao idadi kubwa ni watalii wa ndani.
“Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu, tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini, India, Marekani,Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,alisema Tesha.
Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea ambayo ni ya lami,ukifika Songea mjini eneo la Msamala unasafiri kwa barabara kilometa 3.5 unakuwa umefika bustani ya Luhira.
Malazi ya wageni yanapatikana Manispaa ya Songea ambapo wageni pia wanaweza kuweka mahema ya muda katika maeneo yaliyotengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Novemba 15,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.