JESHI la Polisi mkoa wa Ruvuma kupitia kikosi cha usalama barabarani,limeendesha(limetoa) mafunzo kwa madereva wa idara mbalimbali za Serikali wakiwemo madereva wa vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika mkoa huo.
Mafunzo hayo yana lengo la kuwakumbusha uzalendo na kutii sheria,kanuni na taratibu za usalama barabarani kutokana na kuwa vinara wa kuvunja sheria kwa makusudi na chanzo cha ajali nyingi.
Akifungua mafunzo hayo jana,Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma Kamishina msaidizi wa Polisi Joseph Konyo, amewataka madereva hao kuacha tabia ya kuendesha magari kwa mwendo kasi kwa kuwa ni hatari kwa maisha yao na viongozi wanao waendesha.
Amesema, madereva wanatakiwa kutambua kuwa magari ya Serikali yanatokana na fedha za wananchi, hivyo wana wajibu ya kutunza ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa ya kuboresha huduma na kuharakisha maendeleo.
“ukiwa unaendesha gari la Serikali kimsingi wewe ni mtumishi wa umma,kwa hiyo unawajibika kwa namna yoyote kulinda mali ya umma na viongozi unaye mwendesha”amesema Rpc Konyo.
Amesema, baadhi ya madereva wa magari ya Serikali wanatumia vibaya nafasi hiyo kwa kukiuka sheria za barabarani makusudi ikiwemo mwendo kasi na kupita kwenye maeneo yenye alama kama vile vivuko kwa watembee kwa miguu bila kuchukua tahadhari.
Aidha amesema,wakati mwingine madereva wa Serikali wamekuwa watu wenye dharua kwani hata wanaposimamishwa na askari wa usalama barabarani hawataki kusimama,hivyo kuleta taswira mbaya kwa madereva wa magari binafsi na jamii.
Amesema,kitendo cha kutosimama na kuvunja sheria za barabarani kwa makusudi kimekuwa kero kwa watumiaji wengine na kinachafua sana baadhi ya taasisi,kwa hiyo amewataka kubadilika na kuwa mfano mzuri kwa jamii.
Kamanda Konyo amesema, ni matumaini ya Serikali kupitia mafunzo yanayotolewa na Jeshi la Polisi madereva watabadilika na kuepuka kufanya mambo ya ovyo ambayo ni chanzo cha ajali na kuleta madhara makubwa kwao na watu wengine wasiokuwa na hatia.
Amesema, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na vyombo vingine vikiwemo vyombo vya Habari vitaendelea kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara juu ya matumizi sahihi ya alama za barabarani,kuheshimu na kutii sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Ruvuma Salum Morimori amesema,madereva wa serikali wanatakiwa kuwa jicho na kioo kwa watu wengine kwa kutii sheria zilizopo badala ya kuwa watu wa ovyo.
Amesema, madereva ni watu muhimu kwa maisha ya kila siku ya viongozi wa Serikali,kwa hiyo wana wajibu wa kuhakikisha wanaepusha ajali na madhara mengine kama vifo kwa viongozi .
Kwa mujibu wa Morimori,madereva wakizingatia sheria hakutakuwa na vifo wala uharibifu wa mali za Serikali na kusistiza kuwa, Jeshi la Polisi litawachukulia hatua kali madereva wazembe bila kujali anaendesha taasisi ipi ya Serikali.
Ametaja makosa yanayofanywa mara kwa mara na madereva wa Serikali ni mwendokasi,kutosimama kwenye vivuko vya watembea kwa miguu na kutoheshimu alama zilizowekwa, jambo linalochangia kutokea kwa ajali nyingi na kuleta madhara kwa watu wasiokuwa na hatia.
Amesema, kama wataendesha magari kwa kuzingatia sheria na kuheshimu alama za barabarani,basi watabaki salama wao na viongozi wanaowaendesha na kulinda magari ya Serikali yanayonunuliwa kwa fedha nyingi.
“madereva wa Serikali mmekuwa mfano mbaya sana kwa madereva wengine na jamii inayowazunguka,hamtaki kutii sheria wala kuheshimu alama za barabarani,sasa leo nawaambia hakuna mtu aliye juu ya sheria,sisi kama Jeshi tutawachukulia hatua hata kama uko na kiongozi kwenye gari”amesema Morimori.
Akiongea kwa niaba ya wenzake,Geofrey Cloudius kutoka ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Ruvuma amesema, mafunzo hayo ni muhimu sana kwani yamewakumbusha mambo mengi ya kuzingatia wawapo barabarani.
Amesema, ni kweli madereva wa Serikali ndiyo vinara wa kuvunja sheria za usalama barabarani, na amewataka madereva wenzake kubadilika na kutii sheria na kuzingatia alama zilizowekwa ili kuokoa maisha yao,viongozi wanaowabeba pamoja na kulinda magari ya umma.
Cloudius, amelishukuru Jeshi la Polisi kutoa mafunzo hayo kwani yatawasaidia madereva wengi wa Serikali sio kuzingatia sheria tu,lakini hata kuepusha vifo kwa watu wasiokuwa na hatia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.