maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadhimishwa Desemba Mosi kila mwaka kwa mwaka huu 2024 yanatarajiwa kufanyika kitaifa Mkoani Ruvuma katika viwanja vya Majimaji kuanzia tarehe 24 Novemba hadi Desemba Mosi, 2024.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kuekea maandalizi ya siku ya UKIMWI Duniani Kitaifa.
Mhe. Nderiananga amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya udhibiti UKIMWI ambayo ni ajenda ya kidunia, kutathmini muelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI nchini na kutafakari changamoto mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa Virusi vya UKIMWI(VVU).
Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Kaimu Mkuu wa Program Dkt. Riziki Kisonga amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau imejipanga kutoa huduma mbalimbali za Afya katika maadhimisho hayo kuanzia Tarehe 24 Novemba mpaka siku ya kilele tarehe 1 Desemba, 2024.
“Huduma ambazo tutazitoa zinahusisha huduma za elimu juu ya Virusi vya UKIMIWI (VVU) na matumizi sahihi ya dawa na kingatiba kwa makundi maalum bila kusahau watoto waliopo katika mazingira hatarishi ya kupata UKIMWI, upimaji wa VVU na magonjwa muambata ikiwemo magonjwa ya ngono na homa ya ini,” amesema Dkt. Kisonga.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kwa mwaka 2025 inasema ‘Chagua Njia Sahihi Tokomeza UKIMWI’.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.