Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametoa wito kwa taasisi za Umma nchini kutumia mitandao ya kijamii kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na serikali kupitia taasisi hizo.
Akiwasilisha mada juu ya Mkakati wa Mawasiliano kwa Umma mbele ya washiriki wa Mkutano wa 107 wa Mwaka wa Wadau wa Elimu kwa Umma unaoendelea mjini Morogoro Bw. Msigwa amesema matumizi ya mitandao ya kijamii imekua ni kiungo muhimu katika kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ya uhakika baina ya taasisi na wadau wake na wananchi kwa ujumla.
Amebainisha kwamba kutokana na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yaliyopo duniani kote, serikali na taasisi zake haina budi kujiendesha kidijitali katika nyanja nzima ya mawasiliano na kuhabarisha umma ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo na hatimaye kuwafikia wadau wengi zaidi.
Ameongeza kuwa bado taasisi nyingi zinategemea radio, magazeti na runinga kama njia kuu za kufikisha habari na taarifa kwa jamii huku kukiwa na wimbi kubwa la wananchi wanaotegemea mitandao ya kijamii kupata habari mbalimbali hivyo amewataka Maafisa Habari na Mawasiliano wa taasisi zote za Umma kuhakikisha wanafungua akaunti kwenye mitandao hiyo ya kijamii na kuhakikisha wanaitumia kikamilifu ili kuwafikia wadau na wananchi wengi zaidi.
"Unakuta taasisi haina hata akaunti moja kwenye mitandao wa kijamii au kama wanazo basi idadi ya wafuasi haizidi 200, nichukue nafasi hii kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuwa na wafuasi (followers) zaidi ya 2,000 kwenye akauti yao ya Instagram" Amesema Msemaji huyo Mkuu wa Serikali akiitolea mfano Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inavyotumia mitandao ya kijamii katika kuwafikia wadau wake na jamii kwa ujumla.
Aidha, katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa Idara ya Habari MAELEZO amesisitiza kuendelea kuhuishwa kwa tovuti zote za taasisi za Umma na kwamba kwa sasa serikali pamoja na njia nyingine inatumia tovuti hizo katika kupima utendaji kazi wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.