Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekemea tabia ya uvamizi na mtindo wa kubadili matumizi ya ardhi iliyotengwa mahususi kwa ajili ya Utafiti wa Kilimo.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati akifungua maonesho ya Nane nane kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya. Amesema maeneo mengi ya taasisi za utafiti yamevamiwa na kupimwa viwanja jambo ambalo linatishia utafiti wa kilimo na mifugo kwa kuwa vituo vya utafiti vitakosa maeneo ya kutosha ya kufanyia kazi.
Makamu wa Rais amewataka watanzania kutambua kilimo ni sayansi na hivyo utafiti kilimo usipopewa kipaumbele basi mapinduzi ya kilimo yatabaki kuwa ndoto. Amesisitiza umuhimu wa kupima maeneo ya taasisi za utafiti wa kilimo, kupewa hati na kulindwa wakati wote. Vivyo hivyo ameelekeza mamlaka zinazohusika kutenga na kupima ardhi katika maeneo ya uzalishaji wa mbegu na kuyalinda dhidi ya uvamizi.
Vilevile Makamu wa Rais amekemea uwepo wa makundi makubwa ya mifugo yalioingizwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Amesema madhara yake ni makubwa ikiwemo kuharibiwa sana kwa mazingira kuongezeka kwa migororo mingi kati ya wakulima na wafugaji, wanyama kama Tembo kukimbia bugudha ya mifugo na kuhamia kwenye makazi ya binadamu wakiharibu mazao na hata kuua watu. Amezitaka Wizara zote husika na Wakuu wa Mikoa kuchukua hatua thabiti kudhibiti uingizaji mifugo kinyemela katika maeneo yao ya utawala.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuzingatia maelekezo ya wataalam ili kuweza kuzalisha pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira kutokana na kuongezeka kwa matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na kemikali nyingine jambo lenye athari kubwa kwa afya ya binadamu na viumbe hai vingine.
Ameongeza kwamba Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji nchini ikiwemo kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji, ambapo lengo ni kufikia eneo la umwagiliaji la hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025. Pia ametoa wito kwa wananchi kutumia na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia kuleta tija.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili taifa liweze kujitosheleza kwa chakula na kupata fedha zaidi za kigeni kutokana na mazao mbalimbali. Amasema Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa kuwapatia Maafisa Ugani vitendea kazi mbalimbali vikiwemo pikipiki, vifaa vya matibabu, uhimilishaji pamoja na vifaa vya kupima afya ya udongo.
Ameitaka Wizara ya Kilimo na Mifugo kuanza maandalizi ya kuchukua vijana wengine katika programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow - BBT) pamoja na kuziagiza Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi kuona namna bora ya kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili vijana wa JKT wanaojitolea wapewe kipaumbele kushiriki katika programu hiyo.
Makamu wa Rais ameendelea kusisitiza taasisi za fedha na mabenki hapa nchini kuendelea kushusha riba zaidi ili kuwasaidia wakulima na wafugaji. Ameitaka Wizara ya Kilimo na Fedha kufikiria kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya kilimo utakaosaidia kushusha riba kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Amewapongeza watafiti waliosaidia katika upatikanaji wa mbegu na kutoa wito kwa Wizara ya Kilimo kutafuta utaratibu wa kuwapa tuzo vijana na wabunifu wanaotoa suluhu ya mambo mbalimbali katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema sekta ya kilimo inaendelea kuimarika kutokana na juhudi za serikali katika kuinua sekta hiyo ikiwemo kuongezeka kwa bajeti kufikia shilingi bilioni 970 kutoka bilioni 294. Ameongeza kwamba kuimarika kwa sekta hiyo kumepelekea kuzalishwa kwa kahawa tani 80000, tumbaku kilo milioni 120 huku uzalishaji wa pamba ukiongezeka mara mbili. Bashe ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi bilioni 100 ili kusaidia makampuni ya pamba yaweze kununua zao hilo kwa wakulima.
Waziri Bashe amesema maendeleo ya kilimo yanategemea ufanisi katika sekta zingine ikiwemo bandari. Ameongeza kwamba mabadiliko na uwekezaji wa tija katika bandari yanahitajika kwa sasa kwani yatasaidia wakulima katika kusafirisha mazao yao.
Pia amesema kuanzia mwaka 2024 nchi zote za Afrika zitapata mialiko ya kuhudhuria maonesho ya Nane nane huku akisisitiza mialiko hiyo haitahusisha viongozi pekee bali hadi wakulima na wanunuzi wa mazao wa nchi hizo. Ameongeza kwamba kufuatia kupanda hadhi kwa maonesho hayo kuwa ya kimataifa, juhudi mbalimbali zinaendelea ikiwemo kuboresha maeneo yanayotumika kwa ajili ya sherehe hizo kwa kuyajenga ili yawe ya kudumu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.