Waziri wa Afya Mhe. Jesnista Mhagama amesema kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 8.1 mwaka 2023.
Waziri Mhagama amesema hayo Novemba 29, 2024 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la kisayansi la masuala ya UKIMWI pamoja uzinduzi na usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI mwaka 2022 - 2023 uliofanyika Songea mkoani Ruvuma.
Waziri Mhagama amesema usalama wa watoto wanaozaliwa kutopata maambukizi ya VVU hivi sasa ni mkubwa kutokana na jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuwekeza na kutekeleza afua mbalimbali za masuala ya VVU na UKIMWI.
"Nishukuru sana kwa juhudi za wadau wote ambao wanajielekeza katika kuhakikisha maisha yanaendelea kwa WAVIU na watoto wanaozaliwa katika mahusiano mbalimbali hapa nchini wanakua salama," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameishukuru Tume ya Taifa Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) kwa kuendelea kuratibu suala zima la mapambano ya VVU na UKIMWI kwa kutengeneza mikakati unganishi na shirikishi ambayo itasaidia katika kufikia mafanikio na mikakati iliyowekwa.
Waziri Mhagama ametoa wito kwa kila mmoja kushiriki katika kulinda na kuthamini mafanikio yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuondoa unyanyapaa kwa watu wanaishi na maambukizi ya VVU.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo amesema Mkoa huo umepata mafanikio ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi 4.9 mwaka 2022 ikiwa sawa na asilimia 0.7 huku viwango vya kitaifa ikiwa na asilimia 2.8.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.