MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Madaba kutenga maeneo ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya miti.
Kanali Thomas ametoa ushauri huo wakati anazungumza watendaji wa Halmashauri hiyo kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Madaba.
Amesema hali ya hewa ya Madaba inafaa kwa mazao ya miti,parachichi na tangawizi hivyo vikianzishwa viwanda kuongeza thamani ya mazao hayo wananchi watapata faida maradufu. “Anzisheni pia mashamba ya pamoja (block farming) ,wakulima watapata fursa ya kulima zao la aina moja hivyo kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi “, alisema.
Mkuu wa Mkoa pia amewaagiza watendaji kuhakikisha mbolea ya ruzuku inawafikia wakulima jirani na maeneo wanayoishi.
katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaagiza watendaji katika Halmashauri ya Madaba kusimamia utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika ndani ya mkataba.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo ni lazima miradi itekelezwa kwa viwango ndani ya mkataba .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Sajidu Idrisa Mohamed amepongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Halmashauri hiyo.
Amesema hospitali ya Madaba inatarajia kuanza kutoa huduma za afya wakati wowote ambapo serikali tayari imefunga mashine ya X-ray yenye thamani ya shilingi milioni 350.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 serikali imetoa shilingi bilioni 186 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya watumishi 127 katika Halmashauri ya Madaba.
Halmashauri ya Madaba yenye watumishi 616 ina upungufu wa watumishi 407.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.