Timu ya madaktari Bingwa kutoka mikoa ya Ruvuma,Songwe na Mbeya wameanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr. Louis Chomboko amesema ,kambi ya Madaktari bingwa katika Mkoa wa Ruvuma itakuwa ya siku tano kuanzia Aprili 29 hadi Mei 4 mwaka huu.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea (HOMSO)Dr.Majura Magafu amesema,uchunguzi na matibabu hayo yatahusisha magonjwa ya akina Mama,magonjwa ya ndani kama vile shinikizo la damu,kisukari na figo.
Dr. Majura ameyataja magonjwa mengine yatakayochunguzwa ni magonjwa ya watoto,mifupa,upasuaji,macho,kinywa,meno,upasuaji wa midomo sungura,masikio,pua,koo,afya ya akili,ngozi,moyo,mfumo wa chakula na saratani.
Amesema, Wizara ya Afya na TAMISEMI inaendelea kuboresha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kuwatumia madaktari waliopo katika Hospitali za rufaa za mikoa,kanda,taasisi na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa Dr. Majura,lengo kuu la kuwatumia madaktari bingwa waliopo katika Hospitali na taasisi za serikali ni kufikisha matibabu ya kibingwa kwa wananchi wengi na kwa wakati ili zisaidie wanannchi kupata huduma bora na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal Ahmed Abbas Ahmed ameipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika mkoa wa Ruvuma.
Amewataka Madaktari Bingwa,kutowasubiri wagonjwa hadi wafike Hospitali badala yake, wahakikishe wanajikita zaidi katika kutoa elimu inayohusiana na madhara,namna ya kujikinga na pia kuwafuata wananchi waliko jambo litakalowezesha kuwafikia watu wengi.
Amesema serikali itaendelea kuwekeza kwa kutoa fedha na kuajiri wataalam kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge,ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa za kambi hiyo kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu na kupunguza usumbufu wa kufuata huduma mbali na maeneo yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.