Mafunzo ya afya moja yakamilika Mtwara
MAFUNZO ya Afya moja yaliyoshirikisha wataalam mbalimbali kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi yamekamilika Agosti 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Tiffany mjini Mtwara.
Mafunzo hayo ya siku tano yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo FAO.
Wataalam walioshiriki kwenye mafunzo hayo ni wataalam wa afya za binadamu, mifugo, maliasili, mazingira,wanyamapori na wanahabari kutoka wilaya za Namtumbo na Nyasa mkoani Ruvuma na wilaya za Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mafunzo hayo ,Mwezeshaji wa mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dr.Vayan Laizer amesisitiza mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha watalaam hao kufanya kazi kwa Pamoja ili kushirikiana kutatua changamoto za magonjwa ya milipuko.
Dr.Laizer amesema mafunzo hayo yamejenga uelewa namna ya kuunda timu moja kwa Pamoja ili kukabiliana na magonjwa yanayotoka kwa Wanyama Kwenda kwa binadamu au kutoka kwa binadamu Kwenda kwa Wanyama.
“Magonjwa ya milipuko yasipodhibitiwa mapema yanaweza kuleta athari kubwa katika jamii,timu ya afya moja ikishirikiana inaweza kumlinda binadamu dhidi ya magonjwa’’,alisema Dr.Laizer.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dr.Mary Kitambi ametoa rai kwa wataalam waliopata mafunzo ya afya moja,Kwenda kwenye maeneo yao ya kazi kutoa elimu hiyo kwa wataalam ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo.
Hata hivyo amesisitiza timu za afya moja kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mitatu ambayo ni kuratibu,kushirikiana na kuwasiliana kwa wakati.
Valentina Sanga Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa amelishukuru Shirika la kimataifa la FAO kufadhili mafunzo hayo ambayo yatawawezesha watalaam Kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija kubwa.
Naye Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Dr.Khatib Ramadhan ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa na FAO kwa kuwezesha mafunzo hayo ambayo yataleta matokeo makubwa wakati wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Agosti 18,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.