MADINI ya makaa ya mawe yanayochimbwa mkoani Ruvuma yameingiza zaidi ya shilingi bilioni 400 na kutengeneza ajira za watanzania zaidi ya 700.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kiasi hicho cha fedha kimepatikana kutokana na mauzo ya madini ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 3.3 ambayo yameuzwa kuanzia Agosti 2017 hadi Oktoba 2020.
Amesema uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe unafanyika katika wilaya za Songea ,Mbinga na Nyasa na kwamba Mkoa wa Ruvuma una hazina kubwa ya mashapo ya madini ya makaa ya mawe yaliyofanyiwa utafiti na kampuni tatu kubwa za uchimbaji.
“Kwa mujibu wa utafiti huo,Mkoa wa Ruvuma una mashapo ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 457,mashapo hayo tulionayo,tunaweza kufanya uchimbaji kwa miaka 718 bila kumaliza hazina hii’’,amesema Mndeme.
Hata hivyo Mndeme amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 zaidi ya tani 636,000 za makaa ya mawe ziliuzwa ndani na nje ya nchi.
Amesema Mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya vito na dhahabu ambayo yanachimbwa kwa wingi katika wilaya za Tunduru,Songea ,Mbinga na Nyasa.
Mndeme amesema madini ya vito na dhahabu kuanzia Mei 2019 Mkoa ulianzisha masoko ya madini katika wilaya za Tunduru na Songea ambapo hadi sasa zimeuzwa gramu zaidi ya milioni moja zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni saba 7.7 na kwamba watanzania zaidi ya 1000 wamepata ajira kwenye za uchimbaji wa madini hayo.
Amesema Mkoa wa Ruvuma umejenga kituo cha umahiri wa madini ambacho kitawawezesha wachimbaji kupata elimu ya uchimbaji na utambuzi wa madini hayo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Novemba 2,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.