WILAYA ya Tunduru iliyopo mkoani Ruvuma imebarikiwa na utajiri wa madini mbalimbali ya vito vya thamani na dhahabu.
Endapo madini hayo yangesimamiwa tangu yalipoanza kuchimbwa mwaka 1995,wachimbaji wadogo na serikali ingepata mapato makubwa katika mrabaha na kodi zinazotokana na mauzo ya madini hayo.
kipindi cha nyuma kabla ya serikali ya awamu ya tano,sekta ya madini ilishindwa kuwanufaisha watanzania ambapo Rais Dkt.John Magufuli baada ya kuingia madarakani amefanya mabadiliko katika sekta ya madini ikiwemo kufanya marekebisho katika sheria ya madini hali ambayo imesababisha watanzania kuanza kunufaika katika sekta hiyo.
Moja ya vitu ambavyo Rais aliagiza ni kuanzishwa kwa masoko ya wazi ya madini kila Mkoa ambapo katika Mkoa wa Ruvuma yameanzishwa masoko ya madini mawili moja katika wilaya ya Tunduru na soko la Mkoa mjini Songea.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana anasema soko la wazi la madini ya vito na dhahabu la mjini Songea lilifunguliwa Mei 3,2019 na soko la Tunduru lilifunguliwa Mei 27,2019.
Anasema tangu kufanyika kwa ufunguzi wa masoko hayo hadi kufikia Desemba 31, 2019,jumla ya gramu 206,712 za madini ya vito ziliuzwa sokoni zikiwa na thamani ya shilingi zaidi milioni 513.
Anautaja mrabaha uliolipwa kutokana na mauzo hayo ni zaidi ya milioni 32 na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini ni milioni 5.4 na kodi ya huduma kwa Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 1.5.
Kwa mujibu wa Mhandisi Nkana,madini ya dhahabu katika kipindi hicho zimeuzwa jumla ya gramu 24,415.96 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.310 ziliweza kuuzwa katika soko la madini la Songea.
Anautaja mrabaha ambao ulilipwa serikalini kutokana na mauzo ya dhahabu ni zaidi ya shilingi milioni 138 na ada ya ukaguzi iliyolipwa ni zaidi ya milioni 23 na kodi ya huduma iliyolipwa kwa Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 6.9.
“Kwa ujumla katika masoko yote mawili ya Tunduru na Songea tangu kuanzishwa kwa masoko haya hadi kufikia Desemba 31,2019 madini ya vito na dhahabu yaliyouzwa yalikuwa na uzito wa gramu 231,128.2 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.824’’,anasema.
Mhandisi Nkana anautaja mrabaha wa jumla uliolipwa serikalini ambao umetokana na mauzo ya madini ya dhahabu na vito katika kipindi hicho kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 171 na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini ni zaidi ya milioni 28.5 na kodi ya huduma ya jumla iliyolipwa katika Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 8.4.
Hata hivyo Nkana anakiri kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya wazi ya madini ya vito na dhahabu kuna mafanikio kwa sababu kabla ya soko kuanzishwa kulikuwa hakuna takwimu zozote za mauzo ya madini kwa sababu wafanyabiashara wengi walikuwa hawalipi mrabaha na kodi nyingine zinazotakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria na mikataba ya madini.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 23,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.