Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kijiji cha Luangano, kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wananchi wamefurahia neema ya huduma za afya karibu na makazi yao baada ya Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vitta Rashid Kawawa, kukabidhi vifaa tiba na dawa zenye thamani ya Shilingi milioni 14.5 pamoja na mabomba ya maji.
Hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Luangano iliyojengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Mbunge wao ikiwa ni ishara ya ushindi wa mshikamano katika maendeleo ya kijiji hicho.
Zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu ya wananchi waliotoa eneo la ujenzi, wakifyatua matofali na kushirikiana bega kwa bega na Mbunge wao ambaye alichangia Shilingi milioni tano.
Sasa huduma za afya ambazo zilikuwa ndoto ya mbali zimekuwa halisi, wakazi wa Luangano hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu, hasa kina mama wajawazito, watoto, na wazee waliokuwa wakihangaika kwa miaka mingi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Kawawa alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada za pamoja na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alibainisha kuwa zaidi ya Shilingi bilioni sita zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Kata ya Mputa, huku akiwasihi wananchi kuendeleza imani kwake ili aweze kuendelea kuwatumikia kwa moyo wa kujitoa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, Dkt. Aaroon Hyera, alimpongeza Mbunge huyo kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha sekta ya afya, akiweka bayana mafanikio kama ongezeko la magari ya wagonjwa kutoka sifuri hadi matatu na ujenzi wa jengo la kisasa la kupumzikia kina mama wajawazito.
Diwani wa Kata ya Mputa, Mhe. Swalehe Said Motto, pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walimpongeza Mbunge huyo kwa mchango wake katika sekta za elimu, afya, na maji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.