MDAHALO wa kitaifa wa maadili uliondaliwa na Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo kuelekea tamasha la tatu la utamaduni la kitaifa mkoani Ruvuma umeweka maazimio nane kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini.
Akzungumza kwenye majumuisho ya mhadalo huo kwenye ukumbi wa Chandamali mjini Songea,Afisa Utamaduni Mwandamizi wa Kitengo cha Urithi na Maadili ya Taifa wa Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Tito Lulandala ameyataja maazimio hayo kuwa ni wazazi kuwajibika vema katika malezi ya Watoto wao na jamii iweke mkazo Zaidi katika malezi na makuzi yenye maadili.
Maazimio mengine ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ni wanasiasa katika ngazi zote wahamasishe uwajibikaji wa familia na jamii yote kwa ujumla katika kurithisha maadili mema kwa Watoto na vijana, jamii kulinda maadili na kuhakikisha malezi na makuzi bora ili wasiige tamaduni za kigeni.
Afisa Utamaduni huyo ameyataja maazimio mengine kuwa ni wazazi na walezi kuelimisha watoto kuhusu madhara ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya Sayansi na teknolojia ikiwemo mitandao ya jamii,viongozi wa dini kuhakikisha wanaifundisha jamii maadili mema,wazazi kuwa mfano wa kushiriki kwenye matukio ya kijamii ikiwemo mikutano ya wazazi shuleni na wazazi na walezi kuwa karibu na Watoto wao ili kujua changamoto zinazowakabili na kutengeneza mazingira rafiki kwa Watoto ili wataja changamoto zao.
Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mdahalo huo, alikuwa ni Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Damas Ndumbaro ambapo amewataja wazazi na walezi kuwa wanaoongoza kwa kusababisha mmomonyoko wa maadili.
“Taasisi za malezi na makuzi zimebomolewa,familia zimebomolewa,utamaduni umepotea,dini zimeasiwa,tumevunja misingi ya jamii,utamaduni ndiyo kiboko ya mmomonyoko wa maadili,tunaona fahari kuiga mambo ya nje kuliko mambo yetu’’.alisema.
Katika hatua nyingine Ndumbaro amesema Mkoa wa Ruvuma umepewa heshima ya kufanya tamasha la tatu la utamaduni la kitaifa ambalo linafanyika kwa siku nne katika uwanja wa Majimaji Songea kuanzia Septemba 20 hadi 23 mwaka huu.
Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwenye tamasha hilo ambalo litafungwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Septemba 30 mwaka huu.
Katika mjadala huo wananchi wamepata fursa ya kuchangia mambo mbalimbali yanayosababisha mmomonyoko wa madili ambapo Alhaj Hamis Abdalah All amewataja baadhi ya wazazi na walezi kuwa wanasababisha mmomonyoko wa maadili kutokana na tabia wanazozionesha mbele ya Watoto wao hivyo kuwa mfano mbaya kwa familia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoani Ruvuma Dkt.Primius Nkwera amesema maadili mema na upendo vikitawala katika familia vinaweza kupunguza mmomonyoko wa maadili huku akisisitiza sheria ichukue mkondo wake kwa watu wote wanaovunja sheria na kusababisha maadili mabovu.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Mohamed Ally ameshauri kuimarisha malezi,makuzi na maadili ya Watoto ili kurejesha maadili mema katika jamii.
Naye Shehe wa Mkoa wa Ruvuma Ramadhani Mwakilima ameutaja utamaduni na maadili kuwa vinajengwa na dini ambapo amesisitiza mizizi mikuu ya maadili mema ni wazazi na walezi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mathias Tilia amesisitiza ili kuwa na maadili mema mafundisho ya msingi ya malezi kwa Watoto yaimarishwe.
Kwa ujumla jamii nzima wakiwemo wazazi,walezi,viongozi wa dini,walimu,wanasiasa na wadau wote wanatakiwa kusimamia maadili mema ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.