Na Albano Midelo,Namtumbo
TAMASHA kubwa la kutangaza fursa mbalimbali zilizopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma linatarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 22 hadi 23 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya anazitaja baadhi ya fursa katika tamasha hilo ambalo limepewa jina la Namtumbo Kihenge ni kutangaza fursa za uwekezaji kwenye sekta ya utalii kwa kuwa wilaya hiyo pia imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii wa kiikolojia,kihistoria na kiutamaduni.
“Sisi Wilaya ya Namtumbo ni miongoni mwa Wilaya nchini ambazo zimebeba historia kubwa katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika ambao ulipatikana mwaka 1961’’,alisema.
Analitaja eneo la kitongoji cha Mikulumo kata ya Luegu wilayani Namtumbo kuwa lina historia iliyotukuta hapa nchini kwa kuwa ni eneo ambalo alijificha baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere wakati anatafutwa na askari wa wakoloni katika harakati za kudai Uhuru kuanzia Novemba 24 hadi 25,1955.
Anasema ili kulinda urithi wa eneo hilo serikali imeboresha mnara wa kumbukumbu ya Mwl.Nyerere na kwamba kati ya walinzi wanne waliomlinda Baba wa Taifa alipojificha katika eneo hilo mwaka 1955,walinzi watatu wamefariki lakini,mlinzi mmoja mzee Maulid Hassan mwenye umri wa miaka 90 bado yupo hai na anaishi jirani na mnara huo.
Akizungumza namna alivyomficha Baba wa Taifa na kumuokoa kutoka kwa askari wa wakoloni waliokuwa wanamsaka Baba wa Taifa mwaka 1955,Mzee Maulid anasema kipindi hicho akiwa kijana wa umri wa miaka 20 aliambiwa na baba yake mzee Hassan kumficha Nyerere ili asikamatwe na wakoloni .
Anasema wazungu walipofika walimuulizia baba yake na yeye akajibu yupo mjini kwenye mkutano na kwamba kwa siku tatu alikuwa hajarudi nyumbani.
Mzee Maulid Hassan anabainisha kuwa baba wa Taifa alimficha kwenye vihenge vya baba yake vya kuhifadhia chakula ambavyo vilikuwa nyuma ya nyumba yao.
“Nilimficha Nyerere hapa kwenye vihenge wakati huo msitu ulikuwa mnene sana,tangu asubuhi alishinda kutwa nzima kwenye vihenge,mama alimpikia ugali wa ulezi na nyama ya kuku aliupenda sana nilikula naye na kushinda naye kutwa nzima kwenye vihenge,niliamua kwa ujasiri lolote na liwe, kama wazungu wakigundua bora mimi waniue na wamuache Nyerere’’,alisisitiza Mzee Maulid
Hata hivyo alisema muda wote aliokaa na Nyerere alikuwa anazungumzia Tanganyika kupata Uhuru kutoka kwa wakoloni na kwamba katika kipindi hicho yeye ndiye alikuwa mtu wa karibu wa Baba wa Taifa hadi alipochukuliwa jioni na kuondoka akiwa salama kabisa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Luegu Ditha Kayombo amelitaja eneo hilo kuwa lina utajiri wa historia ya Tanganyika kwa kuwa hadi sasa mzee aliyemficha Baba wa Taifa akiwa wilayani Namtumbo katika harakati za kudai Uhuru mwaka 1955 mzee Hassan bado yupo hai na serikali imejenga mnara wa kumbukumbu katika eneo hilo.
Anatoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha eneo hilo kwa kuongeza majengo na wananchi waliopo jirani na eneo hilo wasogezwe pembeni ili eneo hilo libaki kuwa kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere.
Ameishauri Serikali kuhakikisha Mzee Maulid Hassan aliyemficha baba wa Taifa ili kumuokoa na askari wa kikoloni mwaka 1955 anapatiwa huduma za msingi kama vile maji,umeme,huduma ya afya na kujengewa makazi ya kisasa.
Serikali wilayani Namtumbo imeamua kwa vitendo kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha tamasha la Namtumbo Kihenge lililosheheni fursa lukuki za uwekezaji na uchumi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.