MFUMO wa stakabadhi mazao ghalani katika Mkoa wa Ruvuma umewawezesha wakulima kupata fedha zaidi ya shilingi bilioni 28.
Akizungumza wakati anafungua mkutano wa wadau wa mazao ya ufuta,soya na mbaazi kwenye ukumbi wa Songea Club,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kiasi hicho cha fedha kimepatikana katika msimu wa masoko wa mwaka 2020/2021.
Ameyataja mazao yaliuzwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia minada mbalimbali iliyofanyika katika wilaya za Songea,Tunduru na Namtumbo kuwa ni ufuta,soya na mbaazi.
Kwa mujibu wa Mndeme,zao la ufuta kilo 12,234,737 zilizouzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya shilingi bilioni 25,soya kilo 1,499,077 ziliuzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya shilingi bilioni moja na zao la mbaazi kilo 4,260,77 ziliuzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya sh.bilioni 2.585.
“Mfumo wa stakabadhi mazao ghalani umeonesha mafanikio makubwa katika Mkoa wetu,hivyo leo tunafanya tathmini ya msimu wa masoko uliopita 2020/2021 na kuratibu maandalizi ya msimu wa masoko wa 2021/2022 ambapo ununuzi unatarajia kuanza Mei 2021’’,alisema Mndeme.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amesema mfumo huo umeziwezesha Halmashauri kukusanya ushuru kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kupitia zao la ufuta pekee zilikusanywa zaidi ya sh.milioni 954 za ushuru kwenye Halmashauri.
Mafanikio mengine ya mfumo huo ameyataja kuwa ni kufufuliwa kwa vyama vingi vya ushirika,kuongeza ajira na kwamba mfumo umerahisisha ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya mapato ya serikali kuu kupitia TRA.
Awali akitoa taarifa ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi kwenye mkutano huo,Mrajisi Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoani Ruvuma Bumi Masuba ameutaja uendeshaji wa masoko ya mazao hayo,ulifanyika kupitia vyama vya msingi 98 mkoani Ruvuma na kuleta mafanikio makubwa.
Ameyataja maandalizi ya masoko katika mkoa wa Ruvuma msimu wa 20201/2022 kuwa yanaendelea kufanyika kwa mfumo wa stakabadhi za ghalani kupitia vyama vya ushirika.
“Makadirio ya uzalishaji wa mazao hayo katika msimu huu ni ufuta tani 15,437,soya tani 7,844 na mbaazi tani 2,889’’,alisema Masuba.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 13,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.