MFUMO wa stakabadhi ghalani kwenye mazao umewawezesha wakulima mkoani Ruvuma,kujipatia zaidi ya shilingi bilioni 65 kupitia mazao ya ufuta,mbaazi na soya.
Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Bumi Masuba amesema katika misimu mitatu ya kilimo kuanzia 2018/2019 hadi kufikia msimu wa 2020/2021,Mkoa wa Ruvuma kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ulikusanya kilo 27,664,631 na kuwawezesha wakulima kupata kiasi hicho cha fedha.
“Katika msimu wa mwaka 2020/2021 pekee jumla ya minada 29 ya ufuta imefanyika ambapo jumla ya kilo 8,326 za ufuta ziliuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 2,183 za kilo na kuwapatia wakulima jumla ya shilingi bilioni 17,221,852,087’’,alisema Masuba.
Akizungumzia kuhusu zao la soya,Masuba amesema katika kipindi cha misimu mitatu kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021 jumla ya kilo 4,963,088 za soya zilikusanywa na kuuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 3,375 kwa kilo na kuwaingiza wakulima shilingi 5,234,096,169.00.
Hata hivyo amesema katika msimu wa mwaka 2020/2021 pekee jumla ya minada tisa ya soya imefanyika ambayo imewezesha kuuza kilo 1,090,199 za soya zilizouzwa kwa wastani wa bei shilingi 1,327 na kuwapatia wakulima jumla ya shilingi 1,547,202,688.00 na kwamba ununuzii unaendelea.
Kuhusu zao la mbaazi,Mrajisi huyo wa Ushirika amesema katika kipindi cha misimu mitatu mfululizo ya kilimo kutoka mwaka 2019/2020 hadi 2020/2021,jumla ya kilo 5,864,615 za mbaazi zilikusanywa na kuuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 2,491 na kuwapatia wakulima jumla ya shilingi 3,779,134,182.
Hata hivyo amesema katika msimu wa mwaka 2020/2021 pekee imefanyika minada mitatu yenye jumla ya kilo 808,295 za mbaazi zilizouzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 1,252 kwa kilo na kuwapatia wakulima shilingi 1,011,711,013 na kwamba ununuzi unaendelea.
Mfumo wa stakabadhi ghalani mkoani Ruvuma umekuwa ni msaada mkubwa kwa kuwapatia wakulima kipato kikubwa unapotekelezwa ipasavyo kulingana na miongozo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 20,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.