Wadau zaidi ya 70 wa kilimo, biashara na ushirika wamekutana Songea katika mkutano maalum wa kupitia mafanikio na changamoto za mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaotumika kuuza mazao ya wakulima mkoani Ruvuma. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Heritage Cottage Msamala, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mheshimiwa Peres Magiri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Magiri amesisitiza kuwa mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeleta mageuzi makubwa kwa wakulima wa mkoa huo kwa kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kupata malipo kwa uwazi na kwa wakati, endapo utatekelezwa kwa kufuata sheria na miongozo ya kitaifa.
Takwimu zilizowasilishwa kwenye mkutano huo zinaonesha kuwa katika kipindi cha misimu sita mfululizo kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2024/2025, mfumo huo umewezesha mauzo ya jumla ya tani 122,913.3 za mazao mbalimbali. Mazao yaliyouzwa ni pamoja na ufuta tani 59,787.8 kwa wastani wa Sh. 2,745 kwa kilo, soya tani 16,383.5 kwa wastani wa Sh. 1,035 kwa kilo, na mbaazi tani 46,742 kwa Sh. 1,181 kwa kilo.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Magiri, mfumo huo unatekelezwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika chini ya usimamizi wa vyama vikuu vya TAMCU LTD na SONAMCU LTD, ambavyo vimesifiwa kwa kusimamia kwa ufanisi ubora wa mazao na utekelezaji wa minada ya kielektroniki.
Aidha, alionya juu ya vitendo vya utoroshaji wa mazao kabla ya minada rasmi, akisisitiza kuwa vyama vya ushirika lazima viheshimu muda wa kuanza minada na kuhakikisha malipo kwa wakulima yanafanyika kwa wakati. “Wakulima wetu wasikate tamaa na mfumo huu, tunahitaji uwajibikaji na uadilifu kutoka kwa wote wanaohusika,” alieleza Magiri.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka watunza maghala kuzingatia viwango bora vya utunzaji wa mazao kwa mujibu wa miongozo ya Bodi ya Usimamizi wa Maghala, huku akiipongeza TAMCU na SONAMCU kwa mchango wao katika ustawi wa kilimo na uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Mkutano huo umetajwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, vyama vya ushirika na wadau wa sekta ya kilimo, kuelekea kujenga mfumo imara na endelevu wa masoko ya mazao ya kilimo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.