SERIKALI kupitia wizara ya maji,imetoa shilingi milioni 322 kujenga chanzo kipya cha maji cha Mkele ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.
Kaimu meneja wa kitengo cha usambazaji maji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbinga mjini (Mbiuwasa) James Kida alisema,chanzo hicho kina uwezo wa kuzalisha lita 50,000 kwa siku na ujenzi wake umekamilika.
Alisema,walilazimika kujenga chanzo hicho ili kufidia upungufu wa maji uliotokana na utekelezaji wa mradi mpya wa maji wa Lusaka unaohudumia takribani watu wapatao 12,000 kutoka kata tatu za Ruhuwiko,Betherehemu na Matarawe.
“wakati mradi wa maji Lusaka unajengwa kwa kutumia uzalishaji wa maji wa kwanza,baada ya kukamilika kulijitokeza upungufu mkubwa wa huduma ya maji, kwa hiyo chanzo hiki kimejengwa mahususi ili kufidia upungufu uliojitokeza kwenye mradi huo”alisema Kida.
Kida alitaja vyanzo vingine vinavyohudumia wananchi wa mji wa Mbinga ni Ndengu kilichojengwa mwaka 1984 na vyanzo vinne vilivyopo kijiji cha Tukuzi kwenye mlima maarufu wa Lupembe ambavyo vimejengwa mwaka 2018.
Kwa mujibu wa Kida,chanzo hicho kimeanza kutoa huduma na sasa hali ya upatikanaji maji kwa wakazi wa mji wa Mbinga imeongezeka kutoka wastani masaa 8 hadi 15 na kutoa fursa kwa Mbiuwasa kuongeza wateja wapya bila kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa maeneo mengine.
Amewashukuru wananchi kuachia eneo hilo ili litumike kuongeza uzalishaji wa maji,hata hivyo amewataka kuacha kufanya shughuli za kibidamu ikiwemo kilimo ndani ya mita 60 na kuhakikisha wana tunza na kulinda chanzo hicho kwa manufaa ya wananchi wengi na viweze kuwa endelevu.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Mbinga,wameipongeza Mbiuwasa kubuni chanzo kipya cha maji ambacho kimesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika mji huo.
Joseph Kumburu mkazi wa mtaa wa Lusaka alisema,kabla ya maboresho yaliyofanywa na Mbiuwasa upatikanaji wa maji katika maeneo yao haukuwa wa kuridhisha kama ilivyo katika maeneo mengine ya wilaya ya Mbinga.
Amewapongeza wataalam wa Mbiuwasa kwa kazi nzuri waliyofanya katika kutekeleza miradi mipya ya maji ambayo imewezesha kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika mitaa mingi ya mji wa Mbinga na hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kujikita zaidi katika shughuli za uzalishaji mali.
Alisema, awali kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo na maboresho mengine ya miundombinu ya maji yaliyofanywa na Serikali kupitia mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira(Mbiuwasa) upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ilikuwa changamoto kubwa.
Alisema,walitumia kati ya masaa 2 na 3 kupata maji kutoka kwenye visima vya asili na wengine kwenda kuchota kwenye mito ambayo maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.