SERIKALI imetoa kiasi cha Sh.milioni 302 ili kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sabina Lupukila amesema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 246 zimetoka serikali kuu na Sh.milioni 56 zimetolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru.
Lipukila amesema,Sh.milioni 80 zimetumika kujenga bweni,Sh.milioni 50 kujenga nyumba moja ya walimu ya familia mbili,Sh.milioni 60 kujenga uzio na Sh.milioni 56 kwa ajili ya matundu 32 ya vyoo.
Ameeleza kuwa,Sh.milioni 56 zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru, Sh.milioni 41 zimetumika kumaliza ujenzi wa miradi hiyo iliyoanzishwa na serikali kuu na Sh.milioni 15 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Amesema,bweni lina uwezo wa kuchukua watoto 80 na katika awamu ya kwanza litatumika kulala watoto wa kike wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kujenga bweni lingine la watoto wa kiume.
Shule ya Tunduru Mchanganyiko ina wanafunzi 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wa elimu maalum kuanzia darasa la awali hadi la saba ambao wanatoka nyumbani na kwenda shule kila siku.
Hata hivyo amesema,ujenzi wa bweni hilo ni mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na kuboresha mazingira ya elimu ili kuhamasisha watoto kupenda kusoma na wazazi kupeleka watoto wao shule kwa ajili kupata haki yao ya msingi.
“watoto wenye ulemavu sio kwamba hawana ndoto,lakini changamoto kubwa imetokana na mazingira magumu kwa baadhi ya wazazi,natoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wenye mahitaji maalum wawalete watoto wao kwenye shule hii”alisema.
Mratibu elimu Kata ya Mlingoti Mashariki Erith Banda,ameishukuru serikali kujenga bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum na nyumba moja ya kuishi walimu.
Ambilikile Mwandembo Mwalimu wa watoto wenye ulemavu amesema,watoto hao wamegawanyika kwenye makundi matatu ambayo ni wenye ulemavu wa akili,wenye ulemavu wa kusikia,wenye uono hafifu na wenye ulemavu wa ngozi.
Amesisitiza kuwa,watoto wenye ulemavu wanafundishika hivyo wazazi waache kasumba ya kuwaficha watoto hao nyumbani,badala yake wawapeleke shule wakapate haki yao ya msingi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.