Mwenge wa Uhuru 2024 umetembelea miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji mtiririko katika Kijiji cha Lipaya Kata ya Mpitimbi,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea amesema mradi wa maji Lipaya ni miongoni mwa miradi ya maji mitatu inayojumuisha vijiji vya Lipaya,Kizuka na Lipokela.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.4 iliyopangwa kuhudumia wananchi wapatao 10,394 ambapo amesema katika mradi wa maji Lipaya wenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 utahudumia wananchi wapatao 3,886.
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa RUWASA mradi wa maji Kizuka unagharimu Zaidi ya shilingi milioni 730 na mradi wa maji Lipokela unagharimu Zaidi ya shilingi milioni 734 na kwamba miradi hiyo itasogeza huduma za maji safi na salama Jirani na wananchi.
Mwenge wa Uhuru pia umeweka jiwe la msingi katika mradi wa jengo la dharura katika hospitali ya misheni ya Mtakatifu Joseph Peramiho ambapo hadi sasa Zaidi ya shilingi milioni 896 zimetumika kutekeleza mradi huo ambao unatarajia kutumia Zaidi ya shilingi bilioni 1.5 hadi kukamilika.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea pia umefungua bweni katika shule ya sekondari ya Jenista Mhagama ambapo serikali imetoa shilingi milioni 128 kujenga bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.
Mradi mwingine ambao umewekwa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa katika Kijiji cha Lundusi Peramiho ambapo serikali imetoa Zaidi ya shilingi milioni 434 kutekeleza mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa stendi,maduka 36,vyoo matundu nane,jengo la utawala na vibanda viwili vya walinzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.