MBIO za Mwenge wa Uhuru 2024 zimeikubali miradi yote saba yenye thamani ya shilingi bilioni 4.4 iliyoipitia katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mradi wa maji wa Ngumbo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila amesema mradi huo unagharimu Zaidi ya shilingi bilioni 2.5 na utekelezaji wake umefikia asilimia 100.
“Mradi unawanufaisha wananchi 11,080 waliopo katika vijiji sita vilivyopo katika kata za Ngumbo na Liwundi na mradi umepunguza umbali mrefu wa wananchi kutafuta huduma ya maji’’,alisema.
Mradi mwingine ambao umezinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2024 ni mradi wa ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Mbambabay,mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 umegharimu shilingi milioni 500 kujenga lami nyepesi yenye urefu wa kilometa 0.88.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Thomas Kitusi amezitaja faida za mradi huo kuwa ni Pamoja na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara,kupunguza athari za kimazingira kwenye maeneo yanayochukuliwa changarawe na kuongeza mtandao wa barabara za lami katika Wilaya ya Nyasa kutoka kilometa nne hadi 5.1.
Mwenge wa Uhuru pia umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Lovund inayojengwa katika Kata ya Kilosa Mbambabay ambapo hadi sasa mradi umegharimu Zaidi ya shilingi milioni 703 na unatarajia kutumia Zaidi ya shilingi bilioni 1,2 hadi kukamilika.
Mratibu wa Mradi huo Denis Katumbi ameitaja miundombinu iliyojengwa kuwa ni vyumba nane vya madarasa,nyumba tatu za walimu,nyumba ya Mkuu wa shule,jengo la utawala,maabara tatu,matundu ya vyoo 17,maktaba,bwalo la chakula,uzio kuzunguka eneo la shule,taki la maji la lita 5,000 na kichomea taka.
Mwenge wa Uhuru pia umetembelea mradi wa uhifadhi wa mistu wa asili wa Namswea wenye ukubwa wa keta 23,046, ambao umegharimu Zaidi ya shilingi milioni 42.
Msitu wa Namswea unaunganisha kata nne ambazo ni Linga,Lituhi,Mbaha na Ngumbo na utekelezaji wa uhifadhi wa msitu huo umezingatia sera ya mpango shirikishi wa usimamizi wa misitu ambapo vijiji 11 vimeungabishwa kupitia Kamati za Maliasili za vijiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.