Mkoa wa Ruvuma unatarajia kuzalisha na kuuza zao la korosho tani 28,000 katika msimu wa mwaka 2024/2025.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anazungumza kwenye uzinduzi wa masoko ya zao la korosho katika msimu wa mwaka 2024/2025 kwenye mkutano wa wadau wa tasnia ya korosho Mkoa wa Ruvuma uliofanyika kwenye ukumbi wa Skyway mjini Tunduru.
‘’Leo Oktoba 17,2024 tunafungua msimu masoko wa zao la korosho katika Mkoa wa Ruvuma,ni matarajio yangu kila mdau atashiriki vema kufanikisha msimu wa masoko ya zao la korosho’’,alisema.
Amesema katika msimu uliopita wa mwaka 2023/2024 Mkoa wa Ruvuma katika kutekeleza malengo ya kilimo cha zao la korosho ulizalisha jumla ya kilo milioni 26 sawa na asilimia 60.
Ili kuhakikisha zao la korosho linatoa mafanikio kwa mkulima,Mkuu wa Mkoa amekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU kuhakikisha kinasimamia vizuri mfumo wa malipo kwa mkulima na kuhakikisha Halmashauri zinawasimamia maafisa ugani katika zoezi la ukusanyaji mazao.
Maagizo mengine ambayo ameyatoa Kanali Abbas ni Halmashauri na vyama vya ushirika kuhakikisha vinasajili wakulima kwa kuzingatia majina yao halisi,benki zinatumia majina kamili ya wakulima ili kufanya malipo sahihi na wakala wa vipimo kusimamia matumizi ya vipimo sahihi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt,Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoimarisha sekta ya kilimo mkoani Ruvuma likiwemo zao la korosho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred akizungumza kwenye mkutano huo amesema msimu wa mauzo na masoko ya ,korosho wa mwaka 2024/2025 ulifunguliwa rasmi Septemba Mosi 2024.
Amesema minada imeanza rasmi Oktoba 11 mwaka huu mkoani Mtwara na kwamba mnada wa kwanza mkoani Ruvuma unatarajiwa kufanyika Oktoba 29 ambapo amebainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma katika msimu huu unatarajia kukusanya na kuuza korosho kilo 28,000,000.
Amesema Chama Kikuu cha Ushirika kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho imeandaa mafunzo ya udhibiti ubora wa korosho kwa wenyeviti,mameneja,makarani wa vyama vya msingi vya ushirika AMCOS,wajumbe wa Bodi wa chama kikuu na maafisa ushirika wilayani Tunduru ambapo jumla ya washiriki 176 watapata mafunzo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.