UJENZI wa chuo cha ufundi Stadi VETA Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili umekamilika.
Mkuu wa chuo hicho Mhandisi Lulu Chilumba amesema chuo kinatarajia kuanza mafunzo Januari mwakani.
Amesema chuo linatarajia kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha vijana wanapata mafunzo yatakayowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
“Kwa kuanzia tunaanza na kozi sita katika fani za uhazili,ujenzi,umeme,Seremala,ubunifu wa mavazi,ushonaji na ufundi wa magari “,alisema Mhandisi Chilumba.
Hata hivyo amesema fomu za kujiunga na chuo hicho zinatolewa chuoni Nyasa au kwenye tovuti ya VETA ambapo maombi ya kujiunga yameanza Septemba hadi Oktoba mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ametoa rai kwa wananchi wa jimbo lake kukitumia chuo cha VETA Nyasa ambacho serikali imewasogezea mlangoni.
Mhandisi Manyanya amesema kwa miaka mingi wananchi walikuwa wanapata shida ya kusafiri mbali kufuata chuo cha VETA Songea au Namtumbo.
“Kwa niaba ya wananchi wa Nyasa tunaishukuru serikali kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kupitia mradi huu ambao utawanufaisha vijana wa Nyasa’’,alisisitiza Mhandisi Manyanya.
Kukamilika kwa chuo hiki kunaufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa na vyuo vitatu vya VETA ambavyo ni Nyasa,Songea na Namtumbo, katika nchi nzima kuna vyuo vya VETA 46.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.