MKOA wa Ruvuma umejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kavu(Parchment)kutoka tani 19,000 katika msimu 2022/2023 hadi kufikia tani 75,000 ifikapo mwaka 2025.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas amesema hayo , wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa zao la kahawa kanda ya Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoriki Jimbo la Mbinga.
Alisema,wastani wa uzalishaji wa kahawa kavu katika mkoa huo ulishuka kutoka tani 23,000 katika msimu 2021/2022 hadi kufikia tani 19,000 katika msimu 2022/2023.
Kwa mujibu wake, katika mkoa wa Ruvuma Kahawa inazalishwa katika Halmashauri saba ikiongozwa na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na Nyasa huku Halmashauri ya wilaya Tunduru ikiwa ni mdau mkubwa katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Kanal Laban amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kukifanya kilimo kuwa biashara.
Alisema,mkakati huo umewawezesha wakulima kuwa wafanyabiashara na juhudi hizo zimesaidia sana kuongeza usafirishaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi na kukuza kipato cha Wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Laban,amewaomba wadau wote kushikamana katika kuwekeza katika uzalishaji wa zao la kahawa hasa ikizingatiwa kuwa,ni moja kati ya mazao saba ya kimkakati yaliyoanishwa na serikali.
Aidha alisema,umuhimu wa zao la kahawa unatokana na mchango wake katika kipato cha mtu mmoja mmoja,Halmashauri na Taifa kwa ujumla na kutoa wito kwa wadau kuongeza uzalishaji na unywaji wa kahawa kwa afya ambao upo chini kwa wastani wa asilimia 10.
Kuhusu mkakati wa Kitaifa wa miaka mitano wa kuendeleza sekta ya Kahawa 2020-2025 Kanal Laban alisema,serikali ya mkoa inaendelea kutekeleza mkakati huo ikiwani utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inayotaka uzalishaji wa kahawa kuongezeka hadi kufikia tani 300,000 ifikapo mwaka 2025.
Kanal Laban,amewaonya maafisa ushirika kuacha tabia ya kuwanyanyasa na kutoa vitisho kwa viongozi wa vyama vya msingi(Amcos) wanapohitaji kupata ufafanuzi wa miongozo ikiwemo kupitisha nyaraka wakiwataka kutoa rushwa, jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali kuimarisha sekta ya ushirika nchini.
Badala yake,watumie nafasi zao kuwasaidia wakulima kupitia vyama vya msingi(Amcos) na Vyama Vikuu kuwatumikia wananchi ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la kahawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji na maendeleo ya zao la Kahawa Tanzania Kajiru Kissenge, amewapongeza wakulima wa mkoa wa Ruvuma kwa kuongoza katika uzalishaji wa zao la kahawa aina ya Arabika.
Alisema,bodi ya Kahawa Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani elfu72 hadi kufikia tani elfu 80 na kuongeza soko la kahawa Ulimwenguni inayolimwa hapa nchini.
Mjumbe wa Bodi ya Kahawa Tanzania Gottan Haule alisema,Bodi ya Kahawa inatambua mchango mkubwa unaofanywa na wadau wa zao hilo katika mkoa wa Ruvuma ambao ndiyo kinara kwa kuzalisha kahawa aina ya Arabika hapa nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.