Mkoa wa Ruvuma mwezi Machi mwaka huu umeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato kupitia TRA baada ya kukusanya kwa asilimia 159.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza na watendaji wa serikali na Taasisi za umma kutoka wilaya zote tano mkoani hapa,amesema hivi sasa Mkoa wa Ruvuma upo katika mikoa kumi bora inayochangia Pato la Taifa.
“Huwezi kuamini,mwezi Machi mwaka huu,Mkoa wa Ruvuma tumekuwa wa kwanza kitaifa katika ukusanyaji mapato kupitia TRA,tukusanya kwa asilimia 159,haya ni makusanyo ya serikali kuu inahusika mikoa yote nchini’’,alisema Mndeme.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma umekuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato,ambapo kuanzia Julai hadi Desemba 2020,Mkoa wa Ruvuma umekuwa Mkoa wa pili kitaifa katika ukusanyaji wa mapato kupitia TRA na serikali imetoa tuzo kwa Mkoa.
Amempongeza Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma pamoja wafanyakazi wote kwa ujumla kwa kusimamia ipasavyo ukusanyaji mapato kwa kiwango kilicholeta tija licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa mapato.
“Kazi ya kukusanya mapato ni ngumu,ina changamoto nyingi kwa sababu hakuna mtu anayependa kulipa kodi,ukusanyaji mapato ni muhimu kwa maendeleo kwa sababu serikali inatumia fedha zilizokusanywa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara,umeme,elimu na miradi mingine ya kimkakati.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 16,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.