Mkoa wa Ruvuma katika msimu wa mwaka 2024/2025 hadi kufikia Septemba mwaka huu umefanikiwa kuzalisha tani 23,910,703 za kahawa kavu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anazungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kahawa duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Kijiji cha Liganga wilayani Songea.
Hata hivyo amesema katika msimu huu,Mkoa wa Ruvuma unatarajia kuzalisha tani 25,000 ambapo hadi sasa Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya pili katika uzalishaji wa kahawa Tanzania baada ya Kagera.
Amesema katika msimu wa mwaka 2023/2024 Mkoa wa Ruvuma ulizalisha zaidi ya tani 22,000 za kahawa kavu na kwamba katika kuendeleza zao la kahawa ,Bodi ya kahawa imeweka malengo makuu matatu.
Ameyataja malengo hayo kuwa ni usajili wa wakulima wote wa kahawa ili kuwa na mpango sahihi wa kuwahudumia,utoaji wa miche bora kahawa ambapo kwa mwaka huu tayari miche 3,190,000 itatolewa bure kwa wakulima na mpango wa ufufuaji wa mashamba ya miti ya kahawa iliyozeeka.
"Hali ya uzalishaji wa zao kahawa katika Mkoa wa Ruvuma bado una changamoto nyingi,uzalishaji kwa wakulima wengi ni mdogo, wakulima waelimishwe kuwekeza vizuri katika maeneo yao na ufanyike uhamasishaji wa kupanua mashamba na kuanzisha mashamba mapya’’,alisema.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anavyowekeza kwenye kilimo ikiwemo zao la kahawa ambapo hivi karibuni alitembelea shamba la kahawa la AVIV wilayani Songea.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya wa Mkoa wa Ruvuma kwenye maadhimisho hayo ametoa rai kwa wakulima kuuza kahawa yao kwa njia ya mnada ili kupata bei nzuri kulingana na bei ya soko.
Amesema upatikanaji wa mbolea ya ruzuku umesaidia katika uzalishaji wa zao la kimkakati la kahawa mkoani Ruvuma hivyo wananchi wanapata faida kubwa.
Kaulimbiu ya siku ya maadhimisho ya siku ya kahawa Duniani mwaka huu ni Tunza mazingira kwa kilimo endelevu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.