BENKI ya Biashara Tanzania(TCB)imezindua tawi jipya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ikiwa ni jitihada za Benki hiyo kusogeza huduma za kwa wateja wake na wananchi wa wilaya ya Mbinga.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Sabasaba Moshingi alisema, huo ni mwendelezo na mipango ya muda mrefu ya Benki ya Biashara Tanzania kuhakikisha inasogeza na kuboresha huduma mbalimbali kwa Watanzania hasa ikizingatia ni Benki ya Serikali yao.
Moshingi alisema, tawi hilo jipya la Mbinga litarahisisha kutoa huduma za kibenki kwa wananchi hali ambayo itawezesha kuwapunguzia muda wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma zinazotolewa na Benki mbali na makazi yao.
Alisema,Tanzania Commercial Bank(TCB)imezingatia shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa katika wilaya ya Mbinga na wakulima,wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na Bodaboda ambao sasa hawatalazimika kwenda hadi Makao Makuu ya mkoa Songea mjini kufuata huduma kama hapo awali.
Moshingi alieleza kuwa,Benki ya TCB sio kwamba ni kubwa tu bali ni Benki inayotoa mchango mkubwa katika shughuli za kijamii na kiuchumi katika kuinua sekta ya elimu na afya hapa nchini.
Alisema,ndiyo maana imeona umuhimu wa kusogeza huduma zake hadi wilayani badala ya miji mikuu na itaendelea kuwawezesha mawakala wake ambao watasaidia kutoa huduma hizo hadi kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini na kutimiza adhima ya kutoa huduma bora kwa Watanzania wote.
Alisema,katika kipindi cha miaka kumi Benki hiyo imefanya mageuzi makubwa ikiwamo kuongeza idadi ya matawi kutoka 30 hadi 85 na mikopo kutoka Sh.bilioni 60 hadi kufikia Sh.bilioni 760.
Kwa mujibu wa Moshingi, kati ya fedha hizo Sh.bilioni 127 ni mikopo iliyotolewa kwa wanawake ambapo Tawi la Songea limeongoza kwa kutoa mikopo mingi ikilinganisha na matawi mengine nchini.
Alisema, kwa sasa Benki hiyo ina matawi 85,mawakala zaidi ya 4,000 pamoja na mashine za kutolea fedha(ATM) katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha alisema, benki inajivunia kuanzisha huduma mpya kwa wateja wake ikiwamo mikopo kwa wastaafu ambapo ikitokea mkopaji(mstaafu) amefariki Dunia mrithi au familia haitalazimika kulipa ambapo amewasisitiza wastaafu nchini, kutumia fursa hiyo kwenda kupata mkopo na huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki ya TCB.
Moshingi alitaja huduma nyingine mpya ni ile inayofahamika kwa jina la Njoo tukushike mkono na Songesha inayopatikana kupitia Mtandao wa simu wa Vodacom.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,ameipongeza Benki hiyo kufungua Tawi wilayani humo na kutekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kusogeza huduma zake kwa Wananchi wa Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa jumla.
Alisema, ujenzi wa Tawi la kisasa kutasaidia kushawishi watu wengi zaidi kwenda kufungua akaunti na kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo.
Brigedia Jenerali Ibuge alisema,Ruvuma ni mkoa unaokua kwa kasi kubwa kutokana na shughuli za uzalishaji na kimaendeleo,hivyo kufunguliwa kwa Tawi katika wilaya ya Mbinga ni wakati muafaka.
Mkuu wa mkoa,ameishukuru TCB kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima hasa ikizingatia kuwa,asilimia 80 ya wakazi wa mkoa huo wanategemea shughuli za kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo,ameiomba TCB kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuwakomboa vijana na wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa makundi na watu mbalimbali ili kukuza uchumi wa mkoa huo.
Ameshauri Benki hiyo, kusogeza huduma zake hadi maeneo ya vijijini ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma na kutembea na fedha nyingi mifukoni jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wateja wao.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.