Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekagua vyanzo vya maji kwenye miradi ya maji Ndongosi na Liula wilayani Songea na kuagiza vyanzo hivyo kulindwa ili viwe endelevu.
Brigedia Jenerali Ibuge amesikitishwa na uharibifu wa vyanzo hivyo unaoendelea kufanywa na wananchi kwa kulima mazao na shughuli nyingine za kibinadamu hali inayosababisha vyanzo hivyo kuwa katika hatari ya kutoweka.
“Naagiza kila kijiji kuitisha mkutano mkuu wa kijiji,kati ya ajenda zake kuu,iwe ni namna gani ya kukabiliana na tabia hii ya kuharibu vyanzo vya maji,nimeona miti inavyoangushwa kama haina mwenyewe’’,alisema RC Ibuge.
Hata hivyo alisema serikali inapenda watu wajipatie kipato kutokana na kilimo,ametahadharisha kuwa shughuli za kinadamu ndizo zinazoathiri vyanzo vya maji.
Ametoa rai kwa watalaam wote wa maji wakiwemo RUWASA na Bonde la Maji la Ziwa Nyasa,waende vijijini ili kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi na kuweka ramani kwenye eneo zima ambalo lenye vyanzo vya maji ambapo ameagiza utekelezaji wa maagizo hayo ufanyike kabla ya Desemba Mosi mwaka huu.
“Tusiseme tuna changamoto ya tabianchi ni sisi wenyewe ndiyo tunaoharibu kwa kukamata miti,kulima hadi kwenye kingo za mito ,tunachoma moto misitu na kuvunja sheria mbalimbali za mazingira’’,alisema RC Ibuge.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ya kijiji cha Ndongosi na Liula kwa Mkuu wa Mkoa,Meneja RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles alisema mradi wa maji Ndongosi ulisanifiwa kwa zaidi ya shilingi milioni 332.
Hata hivyo alisema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 23 ni fedha za maandalizi ya mradi,zaidi ya shilingi milioni 51 ni za usimamizi na zaidi ya shilingi milioni 256 ni fedha za ujenzi wa mradi wa maji.
Ameutaja mradi wa maji Ndongosi ulisanifiwa kuhudumia wakazi wapatao 3,175 wenye mahitaji ya maji lita 119,062.5 kwa siku na kwamba chanzo cha maji kutoka mto Mlaimonga kina uwezo wa kuzalisha maji lita 902,016 kwa siku na kwamba mradi umefikia asilimia 98.
Kuhusu mradi wa maji wa kijiji cha Liula,Mhandisi huyo wa maji amesema mradi huo awali, ulisanifiwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja ambapo RUWASA kwa kutumia watalaam wake wa ndani wamefanikiwa kumaliza shughuli zote kwa shilingi milioni 56 ambapo mradi umekamilika na unahudumia watu wapatao 4,320.
Hata hivyo amezitaja changamoto kuu zinazoikabili miradi hiyo ni uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi kwa kuchoma moto hovyo,kulima kwenye vyanzo na kukata miti.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 30,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.