WAZAZI na walezi wanaoishi kata ya Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea,wanatarajiwa kuondokana na adha ya kuwapeleka watoto wadogo maeneo mengine kusoma,baada ya kuanzishwa kwa shule ya msingi Mkombozi (Mkombozi English Medium School).
Shule hiyo inatarajiwa kuanza kudahiri wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza ambao watakuwa wanasoma kwa lugha ya kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili ambalo litafundishwa kwa lugha ya Kiswahili.
Hayo yamesemwa na Mwalimu wa taaluma wa shule ya Sekondari Mkombozi Hills Jackob Kauzeni,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa vitakavyotumika kwa wanafunzi wa madarasa ya awali na msingi kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema.
Alisema,madarasa ya shule ya msingi ni sehemu ya mradi wa shule ya Sekondari Mkombozi Hills ilianza kujengwa mwaka 2020 ambapo uongozi wa shule hiyo uliona kuna sababu ya kuanzishwa kwa shule ya msingi ya Kiingereza (English Medium School).
Alitaja sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa shule hiyo ni baada ya kukosekana kwa shule ya English Medium katika Halmashauri ya wilaya Songea,hivyo wazazi na walezi wengi kulazimika kupeleka watoto wao nje ya Halmashauri kwa ajili ya kufuata masomo.
Aidha alisema,lengo lingine la kuanzishwa kwa shule hiyo ni kuandaa msingi mzuri wa wanafunzi wanaojiunga na sekondari kuendana na kanuni ya ufundishaji na ujifunzaji wa masomo mbalimbali yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza.
Aliongeza kuwa,hadi sasa majengo mawili yenye jumla ya vyumba vya madarasa sita na ofisi mbili yanaendelea kujengwa ambapo ujenzi wake unatarajiwa utakamilika mwezi Disemba mwaka huu.
Alisema, katika ujenzi wa mradi huo wa shule ya msingi fedha zilizopangwa kutumika ni zaidi ya Sh.milioni 95 na mara baada ya kukamilika wataanza kudahili wanafunzi wa madarasa ya awali na darasa la kwanza.
Shule ya Mkombozi iliyopo kijiji cha Kizuka,kata ya Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea,inamilikiwa na mkazi wa kijiji hicho Franco Nditi, aliyeamua kutumia sehemu ya fedha zake zinazotokana na kilimo cha mahindi kujenga na kuanzisha shule miaka sita iliyopita.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema,amempongeza Nditi kwa kuamua kuwekeza fedha zake kujenga shule ambayo itasaidia jamii ya wakazi wa kata hiyo na wilaya ya Songea kupata sehemu sahihi ya kupeleka watoto wao kupata elimu bora.
Mgema,amewaomba wazazi na jamii kwa ujumla kumuunga mkono Nditi kwa kupeleka watoto wenye umri wa kuanza elimu ya awali,shule ya msingi na Sekondari katika shule hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kufundisha kwa lugha ya Kiingereza.
Mkuu wa wilaya alisema, ili kuendana na dunia ya ushindani ambayo inahitaji ushindani mawasiliano ni vema mtu akafahamu angalau lugha mbili za kimataifa ambazo zitamuwezesha kuwasiliana na mataifa mengine.
Pia alisema,mzazi au mlezi anatamani sana kuona mtoto anapata elimu bora,hivyo ameisifu shule hiyo namna ambavyo inatambua kuwaanda wanafunzi wake kwenye misingi bora ya elimu.
“Niwapongeze sana uongozi na walimu wa shule hii kwa namna mnavyojitahidi kutoa elimu ambayo imeambatana na misingi ya malezi yaliyobora”alisema Mgema.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.