MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,amewaagiza viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani humo Tamcu Ltd,kuanza minada ya zao la ufuta ili kuwasaidia wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri.
Alisema,kuanza kwa minada kutazuia wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kwenda kwa wakulima ili kununua zao hilo kwa mfumo usiokuwa rasmi wa kangomba unaowakandamiza na kuwanyonya wakulima.
Mtatiro ametoa agizo hilo , wakati akizungumza na wenyeviti wa vyama vya ushirika vya msingi(Amcos)na viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu)katika kikao kazi kabla ya kuanza
kwa msimu wa ununuzi wa mazao wilayani humo.
Alisema,kwa kuwa wakulima wengi wameshavuna ufuta mashambani hakuna sababu ya kuchelewa kufanyika kwa minada ili wakulima wapate fedha mapema ili ziweze kuwasaidia kufanya maandalizi ya msimu ujao.
Mkuu wa wilaya,amewasisitiza viongozi wa Amcos kuhakikisha wanaajiri makalani wenye sifa,waadilifu,wenye huruma na wakulima na wachapakazi ambao watakwenda kusimamia sekta ya ushirika.Amewataka wasimamizi wa vyama vya msingi vya ushirika kuacha kufanya kazi kwa mazoea,bali kuhakikisha wanabuni vyanzo vipya vitakavyoongeza mapato ili vyama vyao viweze kujiendesha na kuimarika kiuchumi badala ya kutegemea ushuru na makato yanayotokana na mauzo ya mazao.
Mtatiro amewaonya maafisa ugani wilayani humo,kuacha mara moja tabia ya kuzurura mjini wakifanya sterehe na kuacha kwenda vijijini kuwasaidia wakulima kwani kufanya hivyo ni kosa na wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika hatua nyingine Mtatiro amesema,kuanzia msimu wa kilimo 2023/2024 dawa za kupulizia korosho zitafikishwa moja kwa moja kwenye vyama vya msingi(AMCOS) ambavyo vitahusika kugawa viuatilifu kwa wanachama wao,badala ya utaratibu uliotumika katika msimu 2022/2023 wa kupeleka kwa viongozi.
Alisema,utaratibu wa msimu uliopita haukuwa mzuri kwa sababu baadhi ya wakulima hawakupata viuatilifu kwani kuna viongozi waliuza kwa watu ambao siyo wanachama wala wakulima kutokana na tamaa ya kupata fedha.
Mtatiro,amewapongeza wakulima kutokana na jitihada kubwa wanazofanya mashambani licha ya changamoto nyingi wanazopitia,hata hivyo amewakumbusha kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo mapema kwa kupalilia mashamba ya korosho na hata kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu)Imani Kalembo alisema,wameshaanza maandalizi ya msimu mpya kwa kusambaza viroba katika vyama vyote vya msingi kwa ajili ya kukusanya ufuta kutoka kwa wakulima kwenda kwenye maghala.
Ametoa wito kwa viongozi wa Amcos,kuanza mara moja kazi ya kukusanya ufuta na kuhakikisha ufuta wote unaofikishwa kwenye maghala unakuwa safi na wenye ubora kabla ya kufanyika kwa mnada.
Alieleza kuwa,kwa msimu wa masoko 2022/2023 Chama Kikuu kiliendesha minada mitano ya zao la ufuta ambapo jumla ya kilo 2,548,815.00 wenye thamani ya Sh.bilioni 7,710,700.00 ziliuzwa
Kalembo alisema, uzalishaji wa zao la ufuta umeongezeka kutoka kilo 2,219,283 msimu wa 2021/2022 hadi kufikia kilo 2,548,815 msimu 2022/2023 ambapo ni ongezeko la uzalishaji kwa asilimia 12.93.
Alisema kuwa,bei ya zao hilo kwa msimu 2022/2023 iliendelea kuimarika na bei ya wastani ilikuwa Sh.3,019 kwa kilo ikilinganishwa na msimu 2021/2022 ambayo ilikuwa Sh.2,298.96.
Alisema,wakulima wameendelea kufurahi mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa na manufaa zaidi baada ya bei ya mazao yanayouzwa kwa mfumo huo kupanda ukilinganisha na misimu ya nyuma ambayo ufuta uliuzwa na kununuliwa kwa mfumo wa soko huria.
Kwa upande wake Mrajisi msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja alisema,mazao yote ya kimkakati ya ufuta,korosho,kahawa na zao maarufu la mbaazi yataendelea kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.