SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maji safi vijijini RUWASA Wilaya ya Tunduru inatekeleza mradi wa maji safi ya bomba wa Mkowela Kata ya Namakambale ambao unagharimu zaidi ya sh.milioni 160.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema ameridhishwa na mradi huo ambao amesema utaimarisha ndoa za wanawake baada ya kuwa kero kwa waume zao kutokana na kuchelewa kutembea umbali mrefu kufuata maji ya visima.
Amesema serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha inapunguza kero ya maji katika Mkoa wa Ruvuma imetoa zaidi ya shilingi bilioni 30 za kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika wilaya zote .
“Hivi sasa mtaondokana na kero ya kupampu maji kwenye visima itakuwa ukifungua koki maji yanatoka haraka ,kwa hiyo utakuwa unatembea umbali mfupi unapata maji unarudi nyumbani’’,alisisitiza Mndeme.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru Primy Damas amesema kati ya fedha ambazo zimeletwa kutekeleza mradi huo ambazo ni zaidi ya milioni 160,hadi sasa zimetumika zaidi ya shilingi milioni 43 na kwamba mradi umefikia asilimia 80 na utakapokamilika utaweza kuhudumia watu 3.000.
Amesema ujenzi wa mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 50,000,nyumba ya mtambo,uchimbaji mitaro na ulazaji wa mabomba ya maji kwa umbali wa kilometa 3.2,ujenzi wa vituo nane vya kuchotea maji,ufungaji wa pampu na kuvuta umeme katika nyumba ya mitambo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 28,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.