MADARAJA 19 na baadhi ya barabara za maungio zimesombwa na maji mkoani Ruvuma kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) mkoani Ruvuma Mhandisi Silivanus Ngonyani wakati anatoa taarifa ya hali ya barabara na madaraja ya Mkoa wa Ruvuma kwa Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Mtela Mwampamba katika daraja la Njoka Kata ya Kizuka Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Mhandisi Ngonyani amesema ili kurejesha mawasiliano ya madaraja na maungio ya barabara zinahitajika Zaidi ya shilingi bilioni 2.2.
Hata hivyo amezitaja juhudi zinazofanywa na TARURA ili kukabiliana na changamoto ya kusombwa madaraja na maungio ni Pamoja na kuwaelekeza wananchi kutumia njia mbadala na kuomba bajeti ya dharura ili kurejesha miundombinu katika hali yake.
Ameyataja baadhi ya maeneo yanahitaji ujenzi wa madaraja mapya ili kuweza kuhimili wingi wa maji unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Miongoni mwa madaraja mapya yaliyojengwa na TARURA ni daraja la Mto Njoka lililopo katika Kata ya Kizuka Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambapo serikali imetoa Zaidi ya shilingi milioni 600 kutekeleza mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100.
Akizungumzia daraja hilo Mhandisi Ngonyani amesema kukamilika kwa daraja hilo ni muendelezo wa kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita ya kuendeleza uboreshaji wa barabara na madaraja na kwamba ujenzi wa madaraja unaendelea katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.
“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika bajeti ya miundombinu ya barabara Mkoa wa Ruvuma umeidhinishiwa Zaidi ya shilingi bilioni 22.5, hadi kufikia Machi 2024,TARURA Ruvuma imepokea Zaidi ya shilingi bilioni 8.3 ambayo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti ya matengenezo ya barabara na fedha za maendeleo’’,alisema.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa daraja la Njoka,Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mtela Mwampamba amesema Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa wa kilimo ambao unapata mvua nyingi ambazo zinaathiri miundombinu ya barabara na madaraja.
Ameutaja Mto Njoka mwaka jana ulikuwa haupitiki kutokana na kutokuwepo daraja la kudumu ambapo serikali kupitia TARURA imetoa fedha za ujenzi wa daraja la kudumu linalounganisha vijiji vya Muhukuru, Mipeta,kizuka,Magagura hadi Matomondo ambapo sasa barabara hiyo itakuwa inapitika kwa mwaka mzima baada ya kukamilisha daraja moja la Mgugusi ambalo linajengwa katika mwaka wa fedha 2024/2024
Kassim Mbunda Mkazi wa Kitongoji cha Mgugusi Kata ya Kizuka kwa niaba ya wananchi anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja la Mto Njoka ambalo limewezesha wanafunzi wanaosoma katika shule ya Ulamboni kuvuka kwenye daraja hilo.
Amesema kwa muda mrefu wanafunzi wengi walikuwa hawaendi shule kwa mwaka mzima kutokana ukosefu wa daraja na kwamba wananchi walikuwa wanapata shida ya kusafirisha mazao kutoka kwenye mashamba yao baada ya mavuno.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.