Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imeendelea kufungua milango ya utalii kwa kuboresha vivutio vya utalii vinavyopatikana katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya amevitaja miongoni mwa vivutio vya utalii vinavyoendelea kuboreshwa kuwa ni bwawa la Chengena lililopo kilometa sita kutoka mjini Namtumbo.
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika kwenye bwawa hilo,Malenya amesema bwawa hilo lenye umbo la ramani ya Afrika limeboreshwa na kuchorwa majina ya nchi mbalimbali za Afrika na bendera zake.
“Mtu yeyote anaweza kuingia kwenye bwawa hili kwa kuingia kwenye boti maalum na kufanya utalii wa ndani,akafika Chad,Algeria,South Afrika, Kenya, Somaria na nchi mbalimbali ambazo zipo ndani ya Afrika’’,alisisitiza DC Malenya.
Amesema wilaya ya Namtumbo imedhamiria kufikisha ujumbe kwa watanzania kuwa hakuna haja ya Kwenda kwenye nchi hizo,wakati unaweza kufika kwenye nchi hizo kupitia bwawa la Chengena Namtumbo.
Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha vivutio mbalimbali vya utalii ili kuvutia watalii wengi kutoka ndani ya Mkoa wa Ruvuma na nje ya Mkoa.
Hata hivyo amesema anawashukuru wadau mbalimbali waliotoa fedha za kuanza kuboresha bwawa la Chengena ambazo zimewezesha kununua mitumbwi kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani kwenye bwawa hilo na kuchora ramani za nchi za Afrika.
Wananchi wilayani Namtumbo walijitokeza kwa wingi kwenye kivutio hicho na kushiriki kwenye michezo mbalimbali ikiwemo kuvutana Kamba na soka ambapo Kaimu Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Namtumbo Shaibu Majiwa amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuboresha kivutio cha bwawa la Chengena na kuhamasisha michezo.
Amesema bwawa hilo lilikuwepo tangu zamani,hata hivyo halikuonekana kama kivutio cha utalii ambapo hivi sasa watalii wanapata fursa ya kufanya utalii kwenye bwawa hilo.
Majua ametoa rai kwa wananchi wa Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanafika kwenye bwawa hilo kufanya utalii wa ndani.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Namtumbo Ndugu Acheni Mwinsheshe Maulid amesema wilaya hiyo imeamua kumuunga mkono Rais kwa kuhamasisha utalii ambapo amesema wilaya hiyo ina vivutio mbalimbali vya utalii vikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kivutio cha eneo la Luegu ambako alijificha Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwl.Julius Nyerere katika harakati za kudai uhuru mwaka 1955.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo amefunga tamasha la MANTRA CUP lililoshirikisha timu nane kwenye mchezo wa soka.
Ligi hiyo iliyofanyika kwenye kivutio cha utalii Chengena ilianza Oktoba 28 mwaka huu na fainali kufanyika Novemba 12,2023 ambapo mshindi wa kwanza timu ya Bamiani FC imepewa shilingi 700,000,kombe na mpira mmoja.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.