Na Albano Midelo,Namtumbo
WANAWAKE wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Ngollo Malenya wamefanya Jukwaa la Mwanamke (Namtumbo Women Forum) lenye lengo ya kumbadilisha mwanamke kifkra na kiuchumi.
Jukwaa hilo limefanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Mtakatifu Agnes Chipole mjini Namtumbo ambapo mamia ya wanawake kutoka mkoani Ruvuma wamefundishwa mada mbalimbali za kuwajengea uwezo kiuchumi.
Akizungumza kwenye kilele cha jukwaa hilo ambalo pia lilihudhuriwa na baadhi ya wabunge kutoka mkoani Ruvuma,Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya amelitaja lengo la Jukwaa hilo kuwa ni kumwezesha mwanamke kiuchumi,kifkra na kimawazo ili aweze kuibadilisha jamii inayomzunguka.
“Nilizundua Jukwaa la Wanawake wa Namtumbo Oktoba 13 ili kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwenye Jukwaa hilo zilitolewa mada mbalimbali za kumwezesha mwanamke kiuchumi’’,alisisitiza Malenya.
Hata hivyo amesema Jukwa hilo limedhamiria kubadilisha Maisha ya mwanamke kifkra na kimawazo ili aweze kujitambua na kupiga hatua kwa kusonga mbele ambapo amesisitiza mwanamke kutambua nguvu aliyonayo ili kuweza kujikimu kiuchumi na kifkra hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Awamu ya Sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Malenya amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka miradi mbalimbali katika wilaya ya Namtumbo ambayo amesema inakwenda kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, umeme, kilimo, afya,maji,miundombinu na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum mkoani Ruvuma Mheshimiwa Jakline Msongozi akizungumza kwenye kilele cha Jukwaa hilo,amewaasa wanawake kuzingatia mafunzo ambayo wameyapata bure ambapo amesema mafunzo hayo yanayoweza kubadilisha Maisha ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma.
Amesisitiza kuwa mafunzo ya kuwejenga wanawake kiuchumi yataleta tija katika kuendeleza familia na kukuza uchumi wa wanawake, amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwainua wanawake wa Tanzania .
Naye Mbunge wa Viti Maalum wanawake mkoani Ruvuma Mheshimiwa Mariam Nyoka amesema hii ni mara ya kwanza mkoa wa Ruvuma kufanya tukio kubwa la Jukwaa la wanawake wa Namtumbo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya.
Amesema Jukwa hilo limewaunganisha sio wanawake wa Namtumbo pekee,bali wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ambapo pia amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo kutumia tamasha la Namtumbo Kihenge,kutangaza fursa mbalimbali zilizopo wilayani Namtumbo.
Nyoka ameshauri wilaya nyingine mkoani Ruvuma ,kuiga mfano wa Wilaya ya Namtumbo kwa kuhakikisha wanafanya majukwaa ya wanawake ili kuwaendeleza wanawake ambao ni shingo ya familia.
Mheshimiwa Vita Kawawa ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo akizungumza kwenye Jukwaa hilo ,amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni nne kujenga sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma iliyojengwa wilayani Namtumbo.
Amesema sekondari hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 wanaonzia kidato cha kwanza hadi cha sita imeanza kuchukua wanafunzi mwaka huu,inakwenda kuwa mkombozi wa Watoto wa kike.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Ruvuma Elizabeth Ngongi amesema jukwaa hilo limewafungua macho wanawake kutokana na mafunzo mbalimbali waliyopata yakiwemo mafunzo ya fursa za kiuchumi,elimu ya biashara,Saikolojia,Falsafa na Theolojia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.