Katika vilima vya kijani vya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kunavuma hadithi ya hekima ya karne tatu iliyopita.
Ni hadithi ya kilimo cha ngoro—mbinu ya asili ya kilimo cha hifadhi ya mazingira iliyobuniwa na wazee wa kabila la Wamatengo waliotokea Malawi karne ya 17. Kupitia ngoro,
Ardhi ya milima ya Mbinga si tu imeendelea kustawi, bali pia imehifadhiwa kutokana na mmomonyoko unaosababishwa na mvua na upepo mkali.
Ngoro ni zaidi ya mbinu ya kilimo; ni urithi wa kizazi hadi kizazi unaotunza rutuba ya ardhi kwa njia za kipekee.
Kwa mujibu wa Ngwatura Ndunguru, Mbunge mstaafu wa Mbinga, lengo la msingi la ngoro lilikuwa kuzuia kuondoka kwa udongo wa juu—tabaka lenye rutuba nyingi.
Wakulima walijifunza mapema kuwa udongo wa chini hauwezi kustawisha mazao vyema, hivyo wakatengeneza mashimo maalumu yanayoweka rutuba, maji, na unyevu ardhini.
Katika mashimo hayo ya ngoro, mkulima hupanda mahindi, maharage au ngano, huku akifyeka na kufukia nyasi ndani ya mashimo.
Udongo wa chini unapopinduliwa kuwa juu na kuchanganywa na mboji ya majani yaliyooza, huongeza rutuba. Mashimo hayo pia hutumika kama kinga ya asili dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na huhifadhi unyevu muhimu kwa ustawi wa mazao.
Wataalam mbalimbali wa kilimo kama Bike (1938), Stenhouse (1994) na Temu na Bisanda (1966) walibaini kuwa Wamatengo walilazimika kutumia ngoro kama njia pekee ya kulinda ardhi yenye miteremko mikali ya Mbinga. Kilimo hicho cha “draft agriculture” kilihusiana pia na uwepo wa mapango ya kale, ambapo watu waliishi na kuendesha kilimo cha kudumu badala ya kilimo cha kuhamahama kilichokuwa na athari hasi kwa mazingira.
Leo hii, kilimo cha ngoro kinasalia kuwa mfano bora wa uvumbuzi wa kiafrika katika kuishi kwa amani na mazingira. Ni urithi wa maarifa, mazingira, na utamaduni—unaostahili kutunzwa, kuenziwa, na kuigwa na vizazi vijavyo kote duniani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.