WATEJA wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini wameungana na Dunia nzima kuadhimisha Juma la Huduma kwa Wateja ambalo limefanyika katika Tawi la NMB mjini Songea.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho hayo Oscar Nyirenda ambaye ni Afisa Mkuu Udhibiti wa Hatari na Utekelezaji kutoka NMB Makao makuu akizungumza katika hafla hiyo amesema kila mwaka Juma la Huduma kwa wateja hufanyika wiki ya kwanza ya Mwezi Oktoba ambapo mwaka huu ni kuanzia Oktoba nne hadi nane mwaka huu.
‘’Maadhimisho ya Juma la Huduma kwa wateja yanafanyika kote ulimwenguni katika Taasisi zote za kifedha na nyinginezo,kauli mbiu ya Huduma kwa wateja mwaka huu inasema nguvu ya huduma’’.alisema Nyirenda.
Hata hivyo amesema ili kuendelea kuwa mbele katika utoaji wa huduma kwa wateja wa NMB, katika maadhimisho hayo kumezinduliwa Hati ya kiapo cha huduma kwa wateja ili kuonesha kwa vitendo nguvu ya huduma kwa wateja.
Nyirenda Ameyataja mambo muhimu yaliyopo katika kiapo hicho ni kuahidi hupatikanaji wa huduma za uhakika ndani ya NMB kwa wateja wote,kuendelea kuwa wasikivu kwa wateja,kuendelea kuwa na uhakika wa kuaminika,kutoa huduma kwa waledi na nidhamu ya hali ya juu na kuendelea kuwa na usalama wa taarifa za mteja ndani ya Benki.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa NMB Bussiness Club mkoani Ruvuma Michael West,ameipongeza NMB kwa kutoa huduma bora na za uhakika ikiwemo kuwapokea na kuwasikiliza wateja wake bila ubaguzi.
Katika hatua nyingine Benki ya NMB imetoa msaada wa mabati 200 ya geji 28 na urefu wa meta tatu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita katika shule ya Msingi Mfaranyaki iliyopo Manispaa ya Songea.
Mwakilishi kutoka NMB Makao makuu Oscar Nyirenda amesema NMB imeamua kutoa msaada huo kwa kutambua janga la madarasa yaliyoezuliwa katika shule hiyo Januari mwaka huu.
Mkuu wa Shule hiyo Majid Ngonyani ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambapo amesema mwaka mmoja uliopita NMB pia ilitoa msaada wa madawati 57 yenye thamani ya shilingi milioni tano katika shule hiyo hivyo kuondoa upungufu wa madawati uliokuwepo.
Imeandikwa na Albano Midelo,Songea
Oktoba 4,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.