BENKI ya NMB imetoa shilingi milioni 100.9 ili kusaidia maendeleo katika sekta za afya na elimu mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Faraja Ngingo kwenye hafla ya kukabidhi madawati kwa shule za msingi Manispaa ya Songea iliyofanyika katika shule shule ya msingi Kiburang’oma ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
Ngingo amebainisha kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 24 zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa vitanda na magodoro katika hospitali ya Halmashauri ya Madaba na shilingi milioni tano zilitumika kutengeneza madawati 50 katika shule ya sekondari Matetereka.
Kulingana na Meneja huyo, shilingi milioni 33.7 zilitolewa katika Wilaya ya Nyasa kwa ajili ya ununuzi wa mabati katika shule za Lundo,Chinula,Limbo,Ndingine,Chiwindi na Nangombo.
Ameongeza kuwa NMB pia imetoa shilingi milioni 22 katika wilaya ya Songea kwa ajili ya kutengenezea madawati 220 katika shule za msingi Legele,Kiburang’oma,Lipupuma,Londoni na Mkuzo.
Ngingo amesema NMB imenunua bati 150 zenye thamani ya shilingi milioni 5.25 kwa ajili ya shule ya msingi Ntungwe wilayani Namtumbo na kwamba NMB imetoa shilingi milioni 10.2 kwa ajili ya vifaa vya hospitali ya wilaya ya Tunduru.
“Sisi kama wadau tunawajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii,tulipopata maombi haya ya kuchangia maendeleo ya elimu ,tuliamua mara moja kuja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo’’,alisisitiza Meneja wa NMB.
Hata hivyo amesema kwa miaka kadhaa NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Ruvuma kwa kujikita zaidi katika miradi ya elimu kuchangia madawati na vifaa vya kuezekea na kwenye afya kuchangia vitanda,magodoro na vifaa vingine vya matibabu.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameipongeza NMB kwa msaada huo mkubwa kwa wananchi wa Ruvuma.
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amejenga miundombinu mingi ya elimu na afya hivyo wadau wengine kama NMB wanapojitokeza kuchangia vifaa kwenye miradi hiyo wanaunga mkono moja kwa moja juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.
Ametoa rai kwa wadau wengine mkoani Ruvuma kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kuchangia maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile ameishukuru NMB kwa kupunguza changamoto ya madawati na meza katika shule za msingi na sekondari Manispaa ya Songea.
Amebainisha kuwa katika shule za msingi zilizopo Manispaa ya Songea kuna upungufu wa madawati 5,863 na katika shule za sekondari za Manispaa ya Songea kuna upungufu wa meza 6,600.
Wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Kiburang’oma Mary Komba na John Haule kwa niaba ya wanafunzi wenzao wameishukuru Benki ya NMB kwa Msaada wa madawati 40 ambayo yamepunguza uhaba wa madawati.
Benki ya NMB imezifikia wilaya zote nchini ikiwa na matawi zaidi ya 230,wakala zaidi ya 20,000 na wateja zaidi ya milioni sita.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.