Benki ya NMB Kanda ya Kusini imeandika historia katika kijiji cha Peramiho A wilayani Songea,mkoani Ruvuma baada ya kuandaa bonanza kabambe la NMB Kijiji Day lililokusanya mamia ya wakazi wa eneo hilo kwa michezo, burudani, na elimu ya kifedha.
Tukio hilo limebeba dhamira kubwa ya kuwafikia Watanzania wa vijijini kwa kuwapelekea huduma za kifedha karibu na maisha yao ya kila siku, kwa lengo la kuwainua kiuchumi na kijamii.
Bonanza hilo lilipambwa na shamrashamra za michezo mbalimbali kama jogging, kuvuta kamba, mbio za magunia, kukimbiza kuku, na mechi za mpira wa miguu na mikono, huku burudani na vicheko vikishamiri kati ya wananchi na wafanyakazi wa benki hiyo.
Katika hekaheka hizo, NMB iliwaelimisha wanakijiji kuhusu umuhimu wa kuhifadhi fedha katika benki na namna ya kuendesha vikundi vya kijamii kwa njia salama na endelevu.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Roman Degeleki, alisema bonanza hilo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kufikisha huduma zake kwa wananchi wa vijijini ambao mara nyingi hukosa fursa ya huduma rasmi za kifedha.
“Tunahakikisha kila Mtanzania, popote alipo, anapata huduma ya kifedha kwa urahisi, salama, na karibu kabisa na makazi yake,” alisema Degeleki.
Wananchi walioshiriki bonanza hilo hawakusita kueleza furaha yao na faida walizopata.
Florence Luoga, kijana mkazi wa Peramiho, alisema michezo hiyo imekuwa chachu ya mshikamano miongoni mwa vijana.
Naye Pludensia Tawete alieleza alivyoelimika kuhusu usalama wa fedha kwa vikundi kujiunga na mfumo rasmi wa benki, badala ya kutegemea mtu mmoja.
Godfrey Lupembe aliweka wazi kuwa elimu hiyo imefungua macho ya wanakijiji kuhusu faida za akiba benki, ikiwemo kupata mikopo kwa maendeleo ya vikundi.
Kwa kuchanganya michezo, elimu ya fedha, na burudani, NMB imedhihirisha kuwa huduma za kifedha si suala la mijini pekee bali ni haki ya kila Mtanzania.
Bonanza la NMB Kijiji Day limekuwa jukwaa la matumaini, mshikamano, na mabadiliko chanya kwa jamii ya Peramiho,Ni muhimu taasisi nyingine za kifedha kuiga mfano huu, ili kujenga taifa lenye usawa wa kiuchumi na maendeleo jumuishi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.