MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Nyasa kwa kuchangia kwa asilimia 100.02 mfuko wa wanawake,vijana na wenye ulemavu.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua kikao maalum cha Baraza la madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kassim Majaliwa mjini Mbambabay.
Amesema Halmashauri hiyo katika kipindi hicho imeweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni 42 sawa na kiasi kilichopangwa kuchangiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019.
“Katika makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka 2018/2019, mlikisia kukusanya shilingi 1,309,108,000.00 na mlifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 1,099,708,811.00 sawa na asilimia 84,hongereni sana’’,alisema Mndeme.
Mkuu wa Mkoa pia ameipongeza Halmashauri ya Nyasa kwa kufanikiwa kupata hati safi kulingana na ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2019,ambapo amesisitiza kuwa hati safi ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mchikamano na ushirikiano baina ya watalaam na madiwani.
Ripoti ya CAG inaonesha kuwa Halmashauri ya Nyasa imefanikiwa kupata hati safi miaka minne mfululizo,kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 ambapo Mndeme ametoa rai kuendelea kupatikana kwa hati safi hizo iwe chache kuongeza bidii zaidi katika kazi ili kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Mkuu wa Mkoa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa Jimson Mhagama kuwalipa mara moja madiwani stahili zao za mwezi Mei na Juni ili waweze kulipwa kabla ya muda wao kuisha.
Katika hatua nyingine Mndeme ameagiza kufufuliwa kwa mazao ya michikichi na kokoa katika wilaya ya Nyasa ambayo hali ya hewa inafaa kwa mazao hayo.
“Taarifa niliyonayo hadi sasa wilaya nzima inalima kokoa hekari 40 tu,haitoshi,hali ya hewa na udongo tulionao ni rafiki katika mazao hayo,nawaomba madiwani na watalaam nipate taarifa ni hekari ngapi zinafaa kwa kilimo cha michikichi ili tuweze kuandaa kwa ajili ya kuleta miche na kupanda msimu huu’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mazao hayo yanakuwa miongoni mwa mazao ya biashara katika Wilaya ya Nyasa na kuwa chanzo cha mapato kwa mkulima na kuunganisha nguvu na mazao ya korosho na kahawa.
Akizungumza katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Lupingo Casbert Ngwata amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kusimamia utendaji kazi wa Halmashauri na kusababisha Halmashauri nyingi kupata hati safi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amelipongeza Baraza la madiwani la Nyasa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kipindi cha miaka mitano na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo .
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI MKOA WA RUVUMA
MEI 30,2020
MBAMBABAY
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.