Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imepokea Mbegu Elfu Arobaini (40,000) za Michikichi kutoka Taasisi ya Utafiti TARI iliyopo Kihinga Mkoani Kigoma, ili kuanzisha kitalu cha miche na kusambaza kwa Wakulima wa Wilayani hapa.
Lengo la Uanzishaji wa kitalu hiki ni kuboresha na utekelezaji wa kilimo cha Mazao ya kimkakati likiwemo zao la michikichi. Halmashauri inalenga kupanda Hekta 240 katika Kata kumi na moja (11) zilizopo mwambao wa Ziwa Nyasa, ili kukabiliana na uhaba wa mafuta na kuwaongezea kipato wananchi.
Akipokea mbegu hizo kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mh.Isabela O. Chilumba amesema “Mbegu hizo ni Ukombozi mkubwa kwa wakulima kwa kuwa mbegu hii ni ya kisasa na inachukua miaka mitatu kuanza kuvuna”. Awali kulikuwa na Mbegu ya kienyeji ambayo ilikuwa ikichukua miaka zaidi ya mitano na kuendelea mpaka kufikia kuvuna.
Mh. Chilumba ameongeza kuwa kwa Ukanda wa mwambao wa Ziwa Nyasa kuna Kata 11 ambazo zina uwezo mkubwa wa kustawisha zao hili la biashara kwa kuwa awali walikuwa wakitegemea Uvuvi pekee, sasa zao hili limekuja kuwakomboa wakulima ili waongeze kipato na kupata mafuta ya kupikia ya Mawese kutokana na zao hili la Mchikichi.
Aidha ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa kuchangamkia fursa ya Kilimo cha Michikichi ili wakuze kipato cha kaya na kutatua tatizo la mafuta ya kupikia Nchini.
Awali Akikabidhi mbegu hizo Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti cha TARI Kihinga, Dkt Filson Kagimbo amesema amefika kukabidhi na kuotesha mbegu hizo kama wakulima wa Nyasa walivyoomba na Wilaya ya Nyasa ni moja kati ya Wilaya ambazo zina udongo na hali ya hewa inayofaa kuotesha zao la Mchikichi, Ikiwa ni Utekelezaji wa Agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa kwa kuitaka TARI kuzalisha na kusambaza Michikichi nchi nzima.
Ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuchangamkia fursa ya kilimo cha Michikichi kwa kuwa Mbegu hii ni ya kisasa na inazalisha mazao mara tano ya michikichi ya kienyeji ambapo kwa hekta inazalisha Tani 4 hadi 5 za Mafuta, ukilinganisha na miche ya kienyeji inayotoa Tani 1.6 ya Mafuta ya kwa hekta pia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa Bw Jimson Mhagama amesema atahakikisha anawasimamia wataalamu wa kilimo ili waweze kuwahamasisha wananchi wazalishe kwa wingi zao la Michikichi.
Baadhi ya Wananchi wa kikundi cha Nuru kutoka Nanungu kijiji cha Likwilu ambao wana Shamba Darasa la mfano kwa ajili ya kuwafundisha wakulima wa zao la Michikichi Wilaya ya Nyasa wameipongeza Serikali Wilayani Hapa kwa juhudi za kuwaletea mbegu hizo na kuwapa mahitaji wanayotaka na Kuboresha Zao la Michikichi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.