RAIS SAMIA ATOA BILIONI 60 KUJENGA BARABARA YA LAMI MBINGA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 60 kujenga kilometa 35 za lami wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Ephatar Mlavi amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara ya lami ya Kitai hadi Lituhi yenye urefu wa kilometa 82.
Hata hivyo amesema kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali kinahusisha ujenzi wa barabara ya lami kwa kipande cha kutoka Kijiji cha Amanimakoro hadi Kijiji cha Ruanda,barabara yenye urefu wa kilometa 35.
Ameutaja mradi huo kuwa ulianza kutekelezwa Juni 15,2022 ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa miezi 18, hivyo kukamilika Desemba 2023 ambapo amemtaja Mkandarasi wa mradi huo kuwa ni kampuni ya China Railway Seventh Group.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kilometa 35 za barabara kwa kiwango cha lami,ujenzi wa madaraja manne,ujenzi wa makalaveti makubwa saba na ujenzi wa makalavati madogo 58 na kwamba hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 24.
“Barabara hii ina umuhimu mkubwa katika usafirishaji wa makaa ya mawe kwa sababu eneo hili lina migodi mingi ya madini hayo hivyo barabara hii itasaidia usafirishaji wa makaa ya mawe Kwenda sehemu mbalimbali nchini ikiwemo bandari ya Mtwara’’,alisisitiza Mhandisi Mlavi.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa barabara hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Laban Thomas amempongeza Mkandarasi kwa kufanya kazi ndani ya mkataba ambapo amesisitiza kazi hiyo ikamilike mapema ili wananchi waanze kunufaika nayo.
Ameitaja barabara ya Kitai-Lituhi kuwa ni miongoni mwa barabara kubwa mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 82 ambayo inategemewa na Mkoa katika kukuza uchumi na kwamba inaunganisha wilaya za Mbinga na Nyasa ,pia inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia wilaya ya Ludewa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua uamuzi wa kizalendo wa kutekeleza mradi huo unaoufungua Mkoa wa Ruvuma kupitia barabara ya Kitai-Lituhi.
meandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Januari 10,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.