MKUU WA MKOA AWAFUNDA WATUMISHI WA UMMA NAMTUMBO
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza watumishi wa umma kuhakikisha siku zote wanafanya kazi kwa kufuata sera, sheria, taratibu na miongozo ya kiutumishi ili kuwatumikia wananchi kwa ufanisi na tija.
Kanali Laban ametoa maagizo hayo wakati anazungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo wakiwa na madiwani katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo mjini Namtumbo.
RC Laban amehimiza watumishi hao kufanyakazi kwa ushirikiano,kuacha majungu na kuishi kwa upendo baina ya watumishi wote.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Chiriku Chilumba kuhakikisha watumishi wanapata haki zao za msingi za kiutumishi,yakiwemo madai na stahiki zao walipwe.
“Natoa wiki mbili kwa DED kuleta taarifa ofisini kwangu ni watumishi wangapi wameshalipwa haki zao na wangapi hawajalipwa kwanini hawajalipwa’’,alisema Kanali Thomas.
Amesema serikali imetoa shilingi bilioni 11 ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Namtumbo hivyo amekemea tabia ya udokozi wa mali ya umma kwa baadhi ya watumishi badala yake wahakikishe wanasimamia ipasavyo miradi yote ya maendeleo.
“Tufanye kazi kwa uadilifu na weledi kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati,tuache wizi wa pesa za miradi,tuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri iweze kujiendesha’’,alisisitiza.
Amesema Namtumbo ina mazao mengi kama ufuta,mbaazi,soya na mpunga hivyo amewaagiza watendaji wa Kata na vijiji wanaokusanya pesa kwa kutumia POS wasimamiwe ili kuhakikisha pesa zote zinaingia serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Chiriku Chilumba ameahidi kutekeleza maagizo na kuwasimamia watumishi wa umma ili watekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na miongozo ya kiutumishi.
Namtumbo ni wilaya ya kwanza kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kujitambulisha rasmi kwa watumishi wa umma tangu alipoteuliwa na Rais hivi karibuni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Apirili 4,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.