MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amekagua ujenzi wa Barabra ya Matomondo-Mlale Jkt katika Halmashauri ya wilaya ya Songea inayojengwa kwa kiwango cha lami na Wakala wa Barabara za vijijini na mjini Tarura wilaya ya Songea.
Ibuge,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuupatia mkoa huo fedha kwa ajili ya kutekeleza na kuboresha miundombinu ya barabara na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo Ibuge alisema,Serikali imeanza mkakati wa kuunganisha maeneo yote ya mkoa huo kwa kujenga barabara za lami kwa lengo la kurahisisha mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Amewaagiza wahandisi wa Tarura wanaosimamia ujenzi wa barabara hiyo, kuhakikisha kazi inakuwa na ubora wa hali ya juu kulingana na fedha zilizotolewa na Serikali ili wananchi wa maeneo hayo waweze kuitumia kufanya shughuli zao za maendeleo na kukuza uchumi.
Amemtaka Mkandarasi anayejenga barabara hiyo Kampuni ya BR&Associates Ltd kufanya kazi usiku na mchana ili kazi ikamilike kwa muda uliopangwa,badala ya kutumia visingizio vinavyoweza kuchelewesha kazi kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kiuchumi na inasubiriwa kwa hamu na wananchi.
Amewataka wananchi kuwa walinzi wa vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo inayotegemewa kuchochea uchumi wa wakazi wa wilaya ya Songea na mkoa wa Ruvuma.
Aidha Mkuu wa mkoa, amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya BP Station-Sangawani yenye urefu wa km 1 inayounganisha kata ya Bombambili na kata ya mjini katika Manispaa ya Songea iliyojengwa kwa kiwango cha lami nyepesi iliyogharimu jumla ya Sh.milioni 584,625,000.00.
Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo Mkuu mkoa, amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kumwaga uchafu kwenye mitaro jambo linaloweza kusababisha barabara hiyo kutodumu kwa muda mrefu.
Ibuge amewaagiza viongozi wa serikali ya mtaa na kata ya Bombambili, kuwachukulia hatua watu wanao haribu kwa makusudi miundombinu ya barabara inayojengwa kwa fedha nyingi za Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Alisema, barabara hiyo itakapokamilika itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi ambao kwa sasa wanateseka kutokana na ubovu hasa nyakati za masika.
Alisema,hali hiyo imesababisha shughuli za maendeleo kukwama kutokana na wananchi kushindwa kusafiri na kusafirisha mazao wanayozalisha kwenda sokoni au maeneo mengine hapa nchini kwa ajili ya kutafuta wateja.
Kwa upande wake Meneja wa Tarura mkoa wa Ruvuma Wahabu Nyamzungu alisema,barabara ya Matomondo-Mlale Jkt kabla ya kuanza ujenzi wake ilikuwa katika hali mbaya kwa kuwa na mashimo mengi makubwa na kusababisha usumbufu kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo kuelekea katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Alisema,barabara ya Matomondo-Mlale Jkt inajengwa na Mkandarasi BR&Associates Ltd kwa gharama ya Sh.bilioni 4 na kazi ya ujenzi imeanza tangu tarehe 14 April na inatarajia kukamilika Mwezi Disemba mwaka huu na hadi sasa kazi zilizofanyika ni upimaji wa barabara km3.5usafishaji barabara na kuondoa tabaka la udongo ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 8.
Alisema,barabara hiyo itakapo kamilika itaondoa kero ya muda mrefu iliyokuwepo na kujengwa kwa lami kutaongeza thamani ya eneo na mali ikiwamo nyumba zinazomilikiwa na wananchi na kuchochea uendelezaji wa makazi na shughuli za uchumi.
Nyamzungu,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara kwa Tarura hali itakayopunguza kwa kiwango kikubwa changamoto za miundombinu ya barabara na madaraja zilizopo kwa sasa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Matomondo Kalua Yasin alisema, kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami itasaidia sana kuboresha maisha ya wananchi wa vijiji vyote ambavyo vitapitiwa na mradi huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.