Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza wadau mbalimbali wa ushirika,kuhakikisha kuwa ushirika unastawi kwa manufaa ya wanachama na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mndeme,ushirika unalindwa na sera na sheria ya ushirika na kwamba wanachama wenyewe ndiyo wasimamizi wa shughuli za kila siku za ushirika ambapo ameagiza katika Mkoa mzima pawe na mpango kabambe wa kusimamia,kuimarisha na kuendeleza ushirika.”Tusiwaruhusu wanaotaka kupindisha sheria ili waue mfumo wa ununuzi wa mazao ya ufuta,mbaazi na soya katika Mkoa wetu,tusiwaruhusu wezi na wabadhirifu kuwa viongozi wa vyama vya ushirika’’,anasisitiza Mkuu wa Mkoa.
Wakulima mkoani Ruvuma wamenufaika na bei kwa utaratibu wa mfumo wa stakabadhi ghalani hali iliyowezesha kuuza mazao kwa bei nzuri na kupata faida. Mndeme anasema kabla ya mfumo huo bei ya Ufuta ilikua shilingi 1,500, Soya Tshs.500 kwa kilo na Mbaazi ilikuwa shilingi kati ya shilingi 100 na 200 kwa kilo moja.Anasema baada ya kuanza kuuza mazao hayo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani Ufuta umepanda bei toka shilingi 1500 hadi 4,110 kwa kilo na kwamba Mauzo hayo yaliwawezesha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kupata kiasi cha shilingi bilioni 24 kutokana na mauzo ya zao la ufuta pekee.
Kulingana na Mndeme. wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika zao la soya walifanikiwa kuuza kilo moja toka shilingi 500 hadi hadi kufikia shilingi 850 kwa kilo moja na mbaazi toka shilingi 150 kwa kilo hadi shilingi 850.
“Mfumo huu wa stakabadhi za ghalani umeleta tija kwa wananchi na hivyo kuongeza uzalishaji kutoka tani 8,000 hadi 10,000 za zao la ufuta na Kufufuliwa kwa vyama vya Ushirika vya kilimo na Masoko kwani kabla ya kuanza mfumo huu vyama vilivyokuwa vinafanya kazi ni 67 na baada ya mfumo huu kuanzishwa vyama vinavyofanya kazi ni 204 ‘’,anasema Mndeme.
Hata hivyo Mndeme anabainisha zaidi kuwa Halmashauri mkoani Ruvuma zimepata na zinaendelea kupata ushuru na kukuza mapato ya ndani ambapo takwimu za uzalishaji na mapato ya wakulima kwa sasa ni rahisi kupatikana na kuwa wazi tofauti na kabla ya utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mfumo wa Stakabadhi ya mazao ghalani katika Mkoa wa Ruvuma unatekelezwa katika mazao sita ambayo ni korosho, Kahawa, Tumbaku, ufuta, mbaazi na Soya na kwamba umeweza kuingiza fedha kiasi cha shilingi 634,797,630,064 kutokana na mauzo hayo.
Mndeme anasema uzalishaji wa mazao yanayouzwa kupitia mfumo wa Stakabadhi ghalani umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo zao la korosho mwaka 2015 uzalishaji ulikuwa tani 11,329,800 zenye thamani ya shilingi 13,594,800,000 ukilinganisha na mwaka 2020 uzalishaji umeongezeka hadi kufikia tani 24,625,824 zenye thamani ya shilingi 65,376,990,905.
“Zao la Kahawa mwaka 2015 uzalishaji ulikuwa tani 17,518,500 zenye thamani ya shilingi 66,570,300,000 na kwa mwaka 2019/2020 uzalishaji ni Tani 15,675,100 zenye thamani ya shilingi 64,048,458.600’’,anasema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa zao la tumbaku kwa mwaka 2016/2017 uzalishaji ulikuwa tani 160,855 zenye thamani ya shilingi 542,323,900 na kwa mwaka 2018/2019 uzalishaji wa tumbaku ulikuwa ni tani 1,247,814.75 zenye thamani ya shilingi 4,101,640,347.
Mndeme amelitaja zao la Ufuta uzalishaji mwaka 2018//2019 ulikuwa tani 8,428,268 zenye thamani ya shilingi 24,882,415,441 na kwa mwaka 2019/2020 uzalishaji ulikuwa ni tani 10,909,667 zenye thamani ya shilingi 23,687,790,987 na kwamba Ununuzi wa zao hili bado unaendelea.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 24,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.