MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,ameziagiza Halmashauri zote nane za mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira la kupanda miti takribani milioni 1.5 kila mwaka.
Kanal Laban ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti wakati akishiriki zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Mibulani kata ya Ruvuma,na shule ya Msingi Mkuzo kata ya Msamala Manispaa ya Songea.
Alisema licha ya mkoa huo kupata mvua za uhakika mwaka hadi mwaka,lakini baadhi ya maeneo yake yanaashiria kuanza kugeuka jangwa kutokana na kasi kubwa ya ukataji miti ovyo usiozingatia uhifadhi wa mazingira.
Kanal Laban,amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma zikiwemo na taasisi na idara za serikali kuendelea kupanda miti kwa wingi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuzuia tishio la mkoa huo na hatari ya kugeuka jangwa na kuwaonya kuacha tabia ya ukataji miti ovyo katika maeneo yao.
Aidha,amewataka Watanzania kuwapuuza watu wanaoubeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kisingizio kuwa hauna faida ambapo ameeleza, katika kipindi cha miaka 59 serikali ya Jamhuri Muuungano wa Tanzania imefanya mambo mengi na makubwa ya maendeleo.
Alisema,Muungano wetu ni nuru na ndiyo uliodumu kwa muda mrefu hasa katika nchi za Afrika ambazo ziliwahi kuungana lakini baada ya muda mfupi zikasambaratika kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Laban,Muungano wetu ndiyo umemtoa hata Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wake amefanya mambo mengi ya maendeleo.
Alisema,tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Watanzania wameshuhudia mabadaliko makubwa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa,miradi ya maji,miundombinu ya barabara na huduma mbalimbai za kijamii zilizowezesha nchi kupiga hatua kubwa ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa,amezindua vyumba viwili vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali(chekechea)katika shule ya msingi Mbulani kata ya Ruvuma vilivyogharimu kiasi cha Sh.milioni 43,460,000 kupitia mradi wa maendeleo wa GPE-LANES 11.
Akizungumza na wanafunzi,walimu na wazazi alisema,ujenzi wa vyumba hivyo umetokana na mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuboresha elimu ya msingi kuanzia elimu ya awali baada ya kufanya vizuri katika ujenzi wa miundombinu kwa shule za sekondari.
Amewataka wazazi na jamii kwa ujumla,kujitolea na kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo badala ya jukumu hilo kuiachia serikali na kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Erick Ndimbo alisema,mradi huo wa ujenzi wa madarasa ya awali ulianza kutekelezwa mwezi Septemba na kukamilika mwezi Disemba mwaka 2022 na umejengwa kwa mfumo wa force akaunti.
Alieleza kuwa,madarasa hayo yameanza kutumika kuanzia mwezi Januari 2023 kwa wanafunzi 216 ambapo kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kupunguza mlundikano wa watoto kukaa katika chumba kimoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.